Thursday, April 7, 2016

JAMII YATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

USHAURI umetolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mkoani Ruvuma kwamba, Halmashauri za wilaya, mji na manispaa  mkoani humo kuanza utaratibu wa kutunga sheria maalum, itakayowabana watu wote wasiotaka kujiunga na mfuko wa  afya ya jamii na bima ya afya.

Abdiel Mkaro, ambaye ni Meneja wa NHIF Mkoani humo ametoa ushauri huo alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya mwamko mdogo wa wananchi kujiunga na mfuko huo, kwa ajili ya kupata huduma bora za matibabu pindi wanapougua.

Halmashauri hizo amezitaka kuhakikisha kwamba zinaongeza dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake ili wanachama waliojiunga na mfuko huo waweze kupata huduma  ipasavyo pale wanapokwenda kupata huduma kutokana na maradhi yanayowasumbua, ambapo baadhi ya maeneo wanachama wamekuwa wakikosa dawa jambo ambalo limechangia  kwa kiasi kikubwa wananchi wengine  kuogopa kujiunga na mpango huo.


Mkaro alisema kuwa endapo wataweka sheria ndogo ambazo zitamtaka kila mwananchi kujiunga na mfuko huo, itasaidia kuongezeka kwa idadi ya wanachama, hivyo kuwa na watu wengi  wenye afya njema ambao watakuwa na uwezo wa kufanya kazi za kujiletea maendeleo.

Alibainisha kuwa baadhi ya maeneo kumekuwa na mwamko mdogo wa wananchi kujiunga na CHF na NHIF, kutokana na vituo vya kutolea matibabu kutokuwa na dawa za kutosha hivyo kuwakatisha tamaa wanachama na wananchi wengine ambao wanatamani kujiunga na mfuko huo.

Licha ya wataalam wa mfuko huo kujitahidi  kutoa elimu kwa wananchi  na makundi mbalimbali ya kijamii, kama vile madiwani wa halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wao kujiunga, hata hivyo bado kuna changamoto kubwa  kwa makundi mengine  ukiachilia madiwani hao ambao wanabanwa moja kwa moja na utaratibu uliowekwa kutokana na kazi zao.

Pia amewataka Wazazi na walezi kujiunga na huduma mpya ijulikanayo kwa jina la Toto afya kadi, kwa watoto  baada ya kuzaliwa hadi  miaka 18 kwa gharama ndogo ya shilingi 50,400 ambayo inatoa fursa kwa mwanachama wa huduma hiyo, kupata matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima.

Huduma  ya Toto afya kadi, inalenga zaidi watoto wadogo ambao wana umri huo wa kujiunga na NHIF  kwa ajili ya kupata matibabu bure wakati wote watakapougua badala ya mzazi kutembea umbali mrefu, kwa lengo la kutafuta matibabu ya mtoto wake.

Pamoja na mambo mengine, alisisitiza kuwa wakati sasa umefika kwa wazazi na walezi kutumia fursa hiyo adimu ya kujiunga na Toto afya kadi kwa kile alichodai kuwa itaweza kumpunguzia gharama  ya matibabu, pale mtoto wake anapougua.

No comments: