Wednesday, April 27, 2016

VITENDO VYA USHIRIKINA SHULE YA SEKONDARI NGWILIZI VYADHIBITIWA BAADA YA WAZEE KUKETI PAMOJA DIWANI AELEZEA MIKAKATI YAKE YA KIMAENDELEO


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

VITENDO vya ushirikina ambavyo vilikuwa vikifanyika katika shule ya sekondari Ngwilizi iliyopo kata ya Kitanda Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, vimedhibitiwa baada ya wazee wa kata hiyo kuketi pamoja na kuzungumzia juu ya kumaliza kero hiyo.

Diwani wa kata hiyo, Zeno Mbunda alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kueleza kuwa muafaka huo ulifikiwa baada ya kukubaliana na wazee hao kwamba, visiendelee kufanyika kwani vimekuwa vikirudisha nyuma maendeleo ya walimu na wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo na kata kwa ujumla.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.
“Wazee wamekwisha kaa vikao na kumaliza tatizo hili, kwa makubaliano kwamba visiendelee kufanyika tena”, alisema Mbunda.

Awali hivi karibuni katika kikao kilichoketi Aprili 2 mwaka huu, ilielezwa kuwa walimu na wanafunzi hao hufanyiwa vitendo vya hovyo nyakati za usiku ambapo huteswa na wakati mwingine wakiwa wamelala, hujikuta wakiwa nje ya nyumba zao wamevuliwa nguo walizovaa mwilini.

Pamoja na mambo mengine, akizungumzia juu ya mikakati ya kimaendeleo aliyojiwekea katika kata hiyo Mbunda alisema kuwa wameunda kamati ya kuendeleza zao la kahawa katika kata hiyo yenye lengo la kuwafanya wananchi wake, waweze kushiriki kikamilifu katika kuendeleza kilimo cha zao hilo na kukuza uchumi wao.


Alifafanua kuwa katika utekelezaji wa suala hilo, anahamasisha pia uundaji wa vikundi vya ujasiriamali ambavyo kupitia Halmashauri ya mji wa Mbinga vitasajiliwa na kuweza kwenda sambamba katika uzalishaji wa zao la kahawa.

“Mpaka sasa katika kata yangu tuna vikundi 31ambavyo baadhi yake vimesajiliwa na vingine bado vipo kwenye mchakato wa usajili, kata ya Kitanda maeneo mengi yanafaa kwa uzalishaji wa zao la kahawa lengo langu la uhamasishaji huu singependa wananchi wangu wajitikite katika uzalishaji wa mazao mengine pekee, bali hata zao hili litawafanya wainue uchumi wao”, alisema.

Vilevile alieleza kuwa kilichobaki sasa ni kujenga ushirikiano kati ya maofisa ugani waliopo katani humo na wakulima, ili kuweza kufikia malengo husika waliyojiwekea.

Kadhalika alibainisha kuwa katika kufanikisha jambo hilo, atafanya mikutano kuzunguka kata hiyo ambayo ina vijiji vitano ambavyo ni Lupilo, Masimeli, Miembeni, Magangwala na Kitanda kwa lengo la kuhamasisha kilimo cha zao la kahawa.
 

No comments: