Thursday, April 21, 2016

TAKUKURU RUVUMA YASEMA HALMASHAURI ZIMESHAMIRI VITENDO VYA RUSHWA

Yustina Chagaka, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma imesema kwamba, katika mkoa huo watumishi wengi wa serikali wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kushawishi na kupokea rushwa kutokana na kuwa watovu wa maadili, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi za kila siku.

Kufuatia hali hiyo, imeelezwa kuwa serikali imeazimia kupambana na vitendo hivyo na kuwaasa watumishi hao, kuzingatia maadili ya kazi zao na wananchi washiriki kikamilifu katika kutoa taarifa pale wanapoona au kusikia kuna harufu ya vitendo vya rushwa.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Ruvuma, Yustina Chagaka alipokuwa akitoa taarifa yake ya utendaji kazi kwa waandishi wa habari, kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.


“Tumekuwa tukitekeleza matakwa ya sheria inayotuongoza kwa kuzingatia majukumu makuu matatu, kuzuia rushwa, kuelimisha umma, kuchunguza tuhuma za rushwa na kushtaki watuhumiwa wanaobainika kujihusisha na vitendo hivi kwa mujibu wa sheria na majukumu haya yanatekelezwa kupitia madawati ya uchunguzi na mashtaka, elimu kwa umma na dawati la utafiti”, alisema Chagaka.

Chagaka alifafanua kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu, ofisi yake imepokea taarifa 82 kutoka kwa wananchi kupitia vyanzo mbalimbali ambapo idara zinazoongoza kulalamikiwa kuwa ni mabaraza ya ardhi na usuluhishi, mahakama, serikali za mitaa, ardhi, afya, elimu, kilimo na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Alisema kuwa mpaka sasa idadi ya kesi zinazoendelea Mahakamani zipo saba, huku akiongeza kuwa katika mkoa huo wilaya ya Mbinga ndiyo inayoongoza kwa vitendo vya rushwa, na kwamba taasisi hiyo imewataka wananchi kutoa ushirikiano wa karibu ili kuweza kudhibiti hali hiyo.

“Taasisi hii ikiwa ndiyo yenye dhamana ya kupambana na rushwa hapa nchini, inawaasa watumishi wote wa serikali kuwatumikia wananchi kwa uadilifu wakizingatia kanuni, taratibu na sheria zilizopo hivyo kwa yule atakayekamatwa hakika tutamwajibisha”, alisema.

Mkuu huyo wa TAKUKURU alibainisha kuwa bado hawajafikia hatua ya kuweza kujivuna kwamba, wanapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi na mamlaka husika pale wanapohitaji kupata nyaraka wakati wanapofanya uchunguzi wa jambo fulani.

Kadhalika akielezea mikakati ya mkoa huo, katika kumaliza kero kwa wananchi hasa kwenye maeneo yanayoongoza kulalamikiwa kwa kushamiri kwa vitendo vya rushwa alisema kuwa, taasisi hiyo inaendelea kufanya tafiti katika idara mbalimbali za umma ambapo watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria dhidi yao, wanajenga mahusiano madhubuti na wadau katika kuhakikisha wanashiriki kikamilifu dhidi ya mapambano ya rushwa na kuelimisha jamii kwa kufanya warsha zinazohusisha utoaji wa elimu husika.

No comments: