Saturday, April 16, 2016

SHIRIKA LA NSSF RUVUMA LAJIPANGA KUTOA ELIMU KWA WADAU WAKE



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

SHIRIKA la Taifa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoani Ruvuma, limejipanga katika kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na watumishi wa serikali kwa kuhamasisha wajiunge na mifuko iliyoanzishwa na shirika hilo, ili waweze kuepukana na ugumu wa maisha pale wanapofikia hatua ya kustaafu utumishi wao serikalini.

Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa shirika hilo mkoani humo, Dominic Mbwette alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea huku akielezea shughuli mbalimbali, zinazofanywa na shirika hilo.

Mbwette alisema kuwa kuna baadhi ya wastaafu wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu na wengine hufariki dunia, kutokana na kukosa huduma za msingi katika maisha yao ya kila siku hivyo ni vyema wajiunge na mfuko huo ili waweze kuondokana na matatizo hayo yanayowakabili.


Kufuatia hali hiyo amewaomba wananchi na wastaafu kujiunga na mifuko iliyoanzishwa na NSSF ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali, ikiwemo ya muda mrefu na muda mfupi.

Aliyataja mafao ya muda mrefu yanayotolewa na shirika hilo kuwa ni Pensheni ya uzeeni, mafao ya mkupuo maalum, Pensheni ya ulemavu na Pensheni ya urithi na kwamba aliendelea kuelezea mafao ya muda mfupi kuwa ni mafao ya uzazi, mafao ya kuumia kazini pamoja na mafao ya mazishi.

Meneja huyo alizitaja changamoto zinazolikabili shirika hilo kuwa ni uelewa mdogo wa jamii, kuhusiana na mifuko ya hifadhi jambo ambalo amedai kuwa shirika hilo limejipanga katika kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa kujiunga na shirika hilo, ili kuweza kuongeza idadi ya wanachama.

Aidha alieleza kuwa pamoja na changamoto hizo, lakini shirika hilo limeweza kupata mafanikio kwa kutoa mikopo kwenye vyama vya akiba na mikopo (AMCOS) mbalimbali mkoani humo, zikiwemo Ngaka, Mahilo, Pilikano, Ngima zote za wilaya ya Mbinga pamoja na Wino Amcos iliyopo Madaba wilaya ya Songea vijijini.

No comments: