Saturday, April 16, 2016

WANANCHI WAILALAMIKIA HALMASHAURI YAO


Haya ni madaraja yanayolalamikiwa na Wananchi wa kijiji cha Mwilamba wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, ambapo ujenzi wake umekuwa ni wa kusuasua. (Picha na Kassian Nyandindi)


Na Kassian Nyandindi,
Njombe.

WANANCHI wa kijiji cha Mwilamba kilichopo katika kata ya Kipengele wilaya ya Wanging’ombe mkoa wa Njombe, wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kwa kutochukua hatua za haraka kukamilisha ujenzi wa madaraja mawili yaliyopo katika kijiji hicho, ambayo hivi sasa yanasababisha washindwe kuendesha shughuli zao za maendeleo. 

Aidha wananchi hao walisema kuwa kwa muda mrefu, madaraja hayo ambayo yalianza kujengwa tangu mwezi Aprili mwaka jana hadi sasa ujenzi wake unaonekana kusuasua, na hawajui ni lini yatakamilika ili huduma zao za maendeleo ziweze kutekelezeka bila kuwepo usumbufu wa aina yoyote.

Walifafanua kuwa madaraja hayo, ambayo yapo katika mto Nang’ano yanaunganisha kijiji cha Mwilamba hadi kwenye barabara kuu ya kutoka Njombe mjini kwenda wilaya ya Makete.

Baadhi ya wananchi ambao waliomba majina yao yahifadhiwe, waliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na hali hiyo ya ujenzi wa madaraja hayo kutokamilika hasa kipindi hiki cha masika, mto huo hufurika maji na wanashindwa kuvuka kwenda ng’ambo ya pili hasa pale wanapokuwa na wagonjwa ambao wanapaswa kwenda nao kupata matibabu kwenye kituo cha afya cha Misheni Kipengele ambacho kipo makao makuu ya kata hiyo.


Pia walieleza kuwa hata magari yanashindwa kwenda kwenye kijiji hicho, na kulazimika kuishia karibu na yanapojengwa madaraja hayo ambayo ujenzi wake umesimama, huwashusha abiria wanaokwenda kwenye kijiji cha Mwilamba ambapo baadaye hulazimika kuvuka kwa kupita kwenye maji ya mto huo jambo ambalo linaleta hofu juu ya maisha yao.

Wananchi hao walibainisha kuwa kijiji hicho ni maarufu kwa kilimo cha viazi mviringo na upasuaji mbao na kwamba wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli hizo, wanashindwa kwenda huko kutokana na madaraja hayo kutokamilika ujenzi wake na kuwafanya wakulima wa viazi na wafanyabiashara wa mbao kushindwa kuendesha shughuli zao ambazo zilikuwa zinawaletea kipato.

Kwa upande wake Afisa mtendaji wa kijiji cha Mwilamba, Jordan Mtewele na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Mkabe Mbilinyi walipozungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari walikiri kuwepo kwa malalamiko hayo ambayo yamefikia hatua kuwa ni kero kubwa kwa wananchi, na waliuomba uongozi wa halmashauri ya wilaya ya wanging’ombe kuchukua hatua za haraka kabla madhara makubwa hayajatokea katika jamii kwa kumuhimiza mkandarasi husika anayejenga madaraja hayo. 

“Tatizo kubwa linalotusumbua kwenye madaraja haya, ni pale panapotokea wagonjwa mahututi ambao wanalazimika kuwasafirisha kwenda kwenye kituo cha afya cha misheni Kipengele au hospitali ya serikali ya wilaya ya Njombe, tunashindwa kufika nao huko hasa pale mto huu ukiwa umefurika maji”, alisema Mkabe Mbilinyi Mwenyekiti wa kijiji hicho.

Naye Diwani wa kata ya Kipendele, Lukemelo Mgaya alipohojiwa alisema kuwa wananchi wa kijiji cha Mwilamba wanakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na madaraja kutokamilika ujenzi wake, na kwamba wamekuwa wakilazimika kuwabeba wagonjwa kutoka kijijini hapo hadi ng’ambo ya mito hiyo kwa kutumia machela kutoka na magari kushindwa kupita kwenye madaraja hayo.

Mgaya alifafanua kuwa kutoka kwenye kijiji hicho hadi makao makuu ya kata ya Kipengele kuna umbali wa kilometa 15, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo ili wananchi waweze kusafiri na kuendesha shughuli zao za kila siku, na kwamba tatizo hilo anatarajia kulifikisha kwenye kikao cha Kamati ya uchumi na fedha ambacho kitaketi Aprili 20 mwaka huu katika halmashauri hiyo.

Vilevile diwani huyo alimtaja Mkandarasi anajenga madaraja katika mto Nang’ano kuwa ni wa kampuni ya ukandarasi ya Ajuwelo Masika iliyopo Mafinga mkoani Njombe, ambapo ujenzi huo haujulikani utakwisha lini.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Meckedezeki Humbe alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana kero hizo alisema ofisi yake haijawahi kupata malalamiko yoyote juu ya ujenzi wa madaraja hayo.

“Ninyi ndio kwanza mnaniambia, mimi sijasikia lolote juu ya malalamiko hayo subirini nikalifanyie kazi”, alisema Humbe.

Hata hivyo Mkuu wa wilaya hiyo, Asumta Mshama alisema ujenzi wa madaraja hayo unaoendelea kufanyika kwenye mto huo ulianza Septemba 9 mwaka jana na kwamba ulitengewa fedha shilingi milioni 552,241,925 na Mkandarasi huyo amekwisha lipwa kiasi cha fedha shilingi milioni 486,329,342 kwa hatua ya kazi aliyoifanya katika mradi huo na kwamba ukamilishaji wa mradi unasubiri mvua zipungue kunyesha ili aweze kuweka kifusi.

No comments: