Sunday, April 3, 2016

MKUU WA WILAYA SONGEA AWATAKA WANANCHI WAKE KUSHIRIKI KWENYE ZOEZI LA UMEZAJI DAWA



Na Julius Konala,
Songea.

MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Benson Mpesya amewaongoza baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea katika zoezi la umezaji dawa kwa  ajili ya kinga na tiba ya magonjwa yaliyosahaulika na yale ambayo hayapewi kipaumbele (NTD) mjini hapa, ikiwemo ugonjwa wa matende.

Mpesya aliwaongoza wananchi hao katika uzinduzi uliofanyika kwenye Zahanati ya gereza la Mahabusu mjini Songea, kwa kumeza dawa hizo za kinga na tiba ya magonjwa ya usubi, mabusha, ngilimaji, trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo.

Akiwahutubia wananchi, wanafunzi wa shule ya msingi Majimaji, walimu, askari magereza na watumishi wengine wa serikali waliojitokeza katika uzinduzi huo, aliwataka kuondoa hofu  na dhana potofu ya kwamba dawa hizo kwamba zina madhara na kuwa na busha sio heshima katika jamii, bali ni matatizo makubwa.

Mkuu huyo wa wilaya aliwahimiza wananchi wengine, kujitokeza kwa wingi katika kushiriki zoezi hilo linaloendelea mjini hapa pindi wataalamu watakapokuwa wanazungukia maeneo mbalimbali, ikiwemo majumbani, shuleni na katika vyuo.


Akizungumza katika zoezi hilo Daktari bingwa wa magonjwa ya macho wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma, aliyejitambulisha kwa jina la Ngohi alifafanua kuwa chanzo kikubwa kinachochangia kuenea kwa magonjwa hayo ni kutokana na uchafu wa mazingira, wakiwemo mbu aina ya Currex ambaye husababisha ugonjwa wa matende pamoja na inzi wadogo wanaoambukiza ugonjwa wa macho (Trakoma).

Kwa upande wake Mratibu wa magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele katika Manispaa ya Songea, Broady Komba alisema kuwa inakadiriwa kuwa watu bilioni moja duniani wameathirika na magonjwa hayo na watu bilioni mbili wapo hatarini kupata maambukizi ambapo kwa upande wa Tanzania, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 43 wapo mbioni kuambukizwa  na watu milioni tano, wamekwisha athiriwa na mojawapo ya magonjwa hayo.

Komba alisema kuwa zoezi hilo litaendeshwa katika zahanati zote za Manispaa ya Songea katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza wameanza April 1 mwaka huu kwa kutoa dawa za kinga na tiba kwa magonjwa hya usubi, matende, ngilimaji na minyoo huku akiongeza kuwa awamu ya pili zoezi hilo litafanyika mwezi Agosti mwaka huu kwa kutoa dawa za kichocho kwa wanafunzi wa shule za msingi huku akiitahadharisha jamii kuacha kuoga, kuogelea kwenye maji yaliyotuama.

No comments: