Thursday, April 21, 2016

WAKULIMA WATAKIWA KUNUNUA PEMBEJEO ZINAZOUZWA NA TFA

Upande wa kulia Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga akihoji juu ya ubora wa pembejeo za kilimo zinazouzwa na TFA ambapo aliwataka wakulima wa wilaya hiyo kwenda katika duka la taasisi hiyo lililopo mjini hapa kununua pembejeo hizo ili waweze kuboresha mashamba yao.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WAKULIMA wa mazao ya chakula na biashara wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujiunga uanachama na Umoja wa Chama Cha Wakulima Tanzania (TFA) ili waweze kunufaika na fursa zilizopo, ikiwemo uzalishaji wa mazao yao kwa ubora unaotakiwa.

Aidha imeelezwa kuwa ndani ya chama hicho, wakulima hao wataweza kupata elimu juu ya kilimo bora cha kisasa, matumizi sahihi ya pembejeo na kuingia mikataba na TFA ambayo baadaye itawawezesha kuwatafutia masoko ya kuuza mazao yao ya chakula na biashara.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya ufunguzi wa duka la pembejeo za kilimo tawi la TFA lililopo wilayani humo.


“Ndugu zangu dhana ya serikali ni kushirikiana na sekta binafsi ili tuweze kuleta maendeleo hapa nchini, tuonyeshe utaalamu wetu katika sekta ya kilimo tuongeze tija kwa wakulima kuwaunganisha kwenye vikundi na kuwapatia elimu husika”, alisema Ngaga.

Pia Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisema kuwa, licha ya wakulima wa wilaya hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi lakini wanakabiliwa na tatizo la kutokuwepo kwa maghala ya kutosha ya kuhifadhia mazao yao, hivyo alitoa ushauri kwa chama hicho kuona uwezekano wa kuongeza ujenzi wa maghala hayo ili kuweza kukidhi mahitaji husika wakati wa mavuno.

Vilevile alipongeza jitihada zilizofanywa na TFA kwa kufanya uwekezaji wa duka la kuuzia pembejeo za kilimo katika wilaya hiyo, kwa kile alichoeleza kuwa wilaya zilizopo nyanda za juu kusini ndiyo zinazofanya uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara.

Awali akisoma taarifa ya maadhimisho juu ya ufunguzi wa duka hilo, Mkurugenzi mtendaji wa TFA hapa nchini, Sarah Lyimo alieleza kwamba hiyo ni taasisi kongwe ambayo ilianzishwa mwaka 1935 kwa lengo la kuwawezesha wakulima wote pale ambapo kuna matawi yake, kusambaza na kuwafikishia pembejeo na zana bora za kilimo zenye ubora wa hali ya juu kwa gharama nafuu.

Lyimo alifafanua kuwa taasisi hiyo hivi sasa ina matawi 12 yaliyopo katika mikoa ya Arusha, Moshi, Tanga, Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Mafinga, Njombe, Mbeya, Mbozi, Babati na Karatu na ina jumla ya wanachama 4,800.

Alibainisha kuwa lengo ni kumuondolea mkulima matatizo ya upatikanaji na matumizi hafifu ya pembejeo na kwamba, imejiwekea mikakati kabambe ya kuwaelimisha wakulima wote hapa Tanzania juu ya kilimo bora na chenye tija.

“Uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara hapa nchini, unakabiliwa na changamoto nyingi na hili linasababishwa na huduma duni za ugani na utafiti wakulima wengi wanalima bila kufuata kanuni za kilimo bora ikiwemo kulima na kupanda kwa mstari, kupalilia kwa wakati, kuweka mbolea na madawa”, alisema Lyimo.

Hata hivyo alisema urasimu uliopo katika upatikanaji wa mikopo kwa wakulima na mikopo hiyo kuwa yenye riba kubwa, ni changamoto ambazo wakulima wadogo na wakati zimekuwa zikiwatesa hivyo kupitia mtandao wa chama hicho cha wakulima, serikali pamoja na wadau wengineo wa sekta ya kilimo wataweza kuwafikia wakulima wengi kwa gharama ndogo na kwa haraka.

No comments: