Monday, April 25, 2016

WALIMU WATAKIWA KUWA MABALOZI WAZURI KATIKA KUPINGA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MJUMBE wa Kamati ya utendaji Taifa, Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Ruvuma, Jema Mapunda ameipongeza serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kutoa elimu msingi bure, ambapo kupitia utekelezaji huo itaweza kuwapa fursa watoto wa kike kupata elimu hiyo hadi sekondari kwa ufanisi mzuri.

Mapunda alisema hayo juzi, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku moja kwa walimu wanawake viongozi wa CWT mkoani hapa, yaliyofanyika mjini Songea.

Alisema kuwa familia nyingi awali zilikuwa zinasomesha watoto wao kwa kuwapa kipaumbele watoto wa kiume, huku wakike wakibaki nyumbani kwa kisingizio cha kukosa ada na michango mbalimbali jambo ambalo hivi sasa limekomeshwa na Rais Dkt. Magufuli.

Alifafanua kuwa walimu wa kike, wanapaswa kuwa mfano mzuri kwenye maeneo yao ya kazi kwa kuwahimiza wazazi wahakikishe kwamba, watoto wao wanawapeleka shule bila kujali kuwa ni wa jinsia gani.

Vivilevile alieleza kuwa mafunzo hayo, yanawapa fursa ya kupata elimu ya sheria ya kazi na ujasiriamali ili walimu hao wanawake toka wanapokuwa kazini wawe wanafanya maandalizi, kujijenga kimaisha kabla ya kustaafu na kwamba baadaye watakapofikia hatua ya kustaafu wasiweze kuwa ombaomba au tegemezi.

Alisema elimu hiyo pia itawawezesha walimu hao, kupunguza changamoto ya kuwa na madeni mengi yasiyokuwa ya lazima na kuwafanya washindwe kutulia kwenye vituo vyao vya kazi na sio vinginevyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Ruvuma, Mrakibu msaidizi wa Polisi Anna Tembo alipozungumza katika mafunzo hayo alisema kuwa ukatili wa kijinsia unaweza kuwa ni kipigo, ngono zisizokuwa na utaratibu na kufanyiwa vitendo vya kinyama hivyo aliwataka walimu hao huko waendako wakawe mabalozi wazuri katika maeneo yao ya kazi.

Anna alieleza kuwa vilevile walimu wanapaswa kupinga mfumo kandamizi unaochangiwa kwa kiasi kikubwa kutoa lugha ambazo sio rafiki kwa jamii, pamoja na mila na desturi kandamizi zipigwe vita.

Alibainisha kuwa walimu wanasaidia kwa kiasi kikubwa kwa mambo mengi, hasa ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaokaa kwa muda mrefu na watoto shuleni tofauti na wazazi wao ambapo wanatakiwa kutoa elimu nzuri kwa wanafunzi hasa wa kike ili waweze kuendana na maadili mema katika maisha yao, yatakayowafanya waepukane na kudanganywa na matendo maovu.

No comments: