Saturday, April 9, 2016

KITUO CHA AFYA MSINDO CHAKABILIWA NA TATIZO LA UKOSEFU WA MAJI



Na Julius Konala,
Namtumbo.

KITUO cha afya Msindo, kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa maji na umeme jambo ambalo linakwamisha utendaji kazi kwa watumishi waliopo katika kituo hicho.

Jimmy Runje ambaye ni Mganga mkuu wa kituo hicho alieleza kuwa wanapohitaji huduma ya maji, hulazimika kuyafuata umbali mrefu na kuwafanya kuwa katika wakati mgumu hasa pale wanapofikia hatua ya kufua mashuka ya kulalia wagonjwa.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mganga mkuu huyo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu, ambaye alitembelea kituo hicho kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali.


Akizungumzia juu ya changamoto ya ukosefu wa nishati ya umeme kituoni hapo, alisema hali hiyo inasababisha shughuli za upimaji  kitengo cha maabara zishindwe kufanyika ipasavyo, kutokana na mashine wanayotumia mionzi ya jua hususan nyakati za usiku kushindwa kufanya kazi vizuri.

Akizungumza na gazeti hili mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la, Folkward Sanga aliiomba serikali kumaliza tatizo la upatikanaji wa dawa hasa katika vituo vya afya, ambavyo vinalaza wagonjwa.

Sanga aliongeza kuwa katika vituo hivyo kumekuwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua ya kunusuru hali hiyo ikiwemo kuwajengea nyumba ili waweze kuondokana na adha ya kupanga uraiani.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Ally Mpenye, amekiri kuwepo kwa upungufu wa madawa alisema kuwa atazungumza na wizara husika kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango cha dawa hizo.

Alisema kuwa halmashauri hiyo, ipo pia katika mpango wa kutatua changamoto nyingine za ukosefu wa nyumba za kuishi waganga katika zahanati na vituo vya afya, vilivyopo wilayani humo.

Kituo cha afya cha Msindo kinahudumia wananchi wa vijiji vinne ambavyo ni Mtakanini, Lumecha, Nambehe na Msindo ambapo kituo hicho kinauwezo wa kulaza wagonjwa 20 hadi 25 kwa siku.

No comments: