Thursday, April 21, 2016

TASAF SONGEA KUNUFAISHA KAYA MASKINI




Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MPANGO wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, unatarajia kunufaisha kaya 5,016 zilizopo katika wilaya hiyo ambazo zitapewa ajira za muda na kunufaika na mpango huo, utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 865,260,000.

Ofisa ushauri na ufuatiliaji wa TASAF katika halmashauri hiyo, Aniceth Kyaruzi, alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake mjini hapa.

Kyaruzi alisema kuwa halmashauri ya wilaya ya Songea, imekwisha anza mchakato wake wa kuibua na kupanga miradi kwa ajili ya kutoa ajira za muda katika vijiji 37 wilayani humo, ambavyo ni miongoni mwa vijiji 48 vinavyotekeleza mpango huo wa kunusuru kaya maskini.


Alifafanua kuwa miradi itakayopewa kipaumbele katika mfuko huo, ni ile yenye manufaa ya muda mrefu kwa jamii hususan katika kukabiliana na changamoto  za mabadiliko ya tabia nchi, mafuriko, ukame na upatikanaji wa chakula.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, walengwa ni wale kaya maskini zilizotambuliwa na kufanyiwa upembuzi yakinifu ambazo zinapokea ruzuku ya kila mwezi ndio watakaokuwa wakifanya kazi hizo na kupewa ujira wa shilingi 2,300 kwa siku 60 katika mwaka.

Aliongeza kuwa mpaka sasa, kuanzia mwezi Septemba 2015 hadi Machi 2016, halmashauri  ya wilaya ya Songea imekwisha toa ruzuku inayofikia kiasi cha fedha za kitanzania, shilingi milioni 848 kwa kaya maskini 6,239 ambazo zinawalengwa wanaofikia 31,195.

Kwa upande wake Mratibu wa mpango huo katika halmashauri hiyo, Hossana Ngunge alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa mpango huo wilayani humo mafanikio mbalimbali yamepatikana ikiwemo kupambana na maadui watatu ambao ni umaskini, ujinga, maradhi, kulipia gharama za matibabu, kuongezeka kwa kipato katika kaya maskini pamoja na kupeleka watoto shule.

No comments: