Friday, April 1, 2016

KAMPUNI YA USAFIRISHAJI ABIRIA KUPUNGUZA ADHA YA USAFIRI RUVUMA



Na Julius Konala,   
Songea.

KAMPUNI ya usafirishaji abiria mikoani inayofahamika kwa jina maarufu la, Ilyana Company Limited ya jijini Dar es salaam, imepanua huduma zake kwa kufungua ofisi zake katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na kufanya idadi ya makampuni ya usafirishaji mjini hapa, kuwa matatu.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni hiyo, Khalfan Kigwenembe alisema kuwa lengo la kufungua ofisi hiyo ni kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Manispaa ya Songea na mkoa kwa ujumla kusafiri kwa bei nafuu ambayo imepangwa na serikali.

Kigwenembe ambaye pia ni Diwani wa kata ya Namtumbo mjini, wilayani Namtumbo mkoani hapa, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alisema kuwa mabasi ya kampuni hiyo yatafanya safari zake kuanzia Songea, Mbinga, Namtumbo hadi  Dar es Salaam.


Amewataka wafanyabiashara wengine wa usafirishaji wa abiria,  kujitokeza kwa lengo la kuwekeza kwenye wilaya zilizofikiwa na miundombinu ya barabara  za lami, na pia kutokana na kukua kwa mkoa huo na idadi ya watu kuongezeka.

“Naiomba Mamlaka ya usafirishaji wa nchi kavu na majini SUMATRA hapa mkoani Ruvuma, kuzingatia haki na usawa katika upangaji wa ratiba ya safari za magari ya abiria bila ya kupendelea kampuni yeyote, kwa kuwa kila mfanyabiashara ana hiari ya kupeleka gari yake mahali popote pale ilimradi anafuata sheria zilizowekwa ndani ya nchi”, alisema Kigwenembe.

Kwa upande wake, Fatuma Msusa mkazi wa maeneo ya Majengo katika Manispaa ya Songea alisema kuwa kuongezeka kwa kampuni hiyo ya usafirishaji kutakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi wa mkoa huo, akidai kuwa awali kulikuwa na adha kubwa ya usafiri pindi shule zinapofungwa kutokana na magari hayo kusafirisha wanafunzi na kuwafanya abiria wengine kusubiri zaidi ya siku tatu, kwa sababu ya uchache wa vyombo vya usafiri uliopo.

Vilevile wananchi wa Manispaa hiyo kwa nyakati tofauti hapa mkoani Ruvuma, wameishukuru na kuipongeza kampuni hiyo kwa kuwasogezea huduma karibu na kuongeza kuwa uwepo wa ushindani, maendeleo hupatikana kwa urahisi.

No comments: