Friday, April 1, 2016

JESHI LA POLISI LAMSAKA ASKARI WAKE ALIYETOROKA BAADA YA KUGHUSHI VYETI VYA MASOMO



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI  la Polisi mkoani Ruvuma,  linamsaka askari wake wa kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia (FFU) mkoani humo mwenye namba F 5425 PC Emmanuel Nyagoli (35) kwa kosa la kutoroka jeshini, baada ya kukabiliwa na tuhuma ya kugushi vyeti vya masomo wakati alipokuwa akijiunga na jeshi hilo mwaka 2003.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani humo Zubery Mwombeji alisema kuwa askari huyo alitoroka tangu Machi 16 mwaka huu, ilipobainika kwamba ametenda kosa hilo.

Mwombeji alisema kuwa PC Emmanuel, alikuwa ni askari wa kikosi cha kutuliza na kuzuia ghasia na kwamba alipogundulika kuwa ana tatizo hilo, ndipo alitoroka na kutokomea kusikojulikana.


Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma, ametoa rai kwa yeyote atakayekuwa na taarifa zinazohusiana na askari huyo mahali alipo, atoe taarifa katika kituo chochote cha Polisi kilichokuwa karibu naye.

Alifafanua kuwa askari huyo, alitoroka na kuacha vitambulisho vyote vya kazi pamoja na sare kwenye nyumba aliyokuwa anaishi yeye na familia yake na kwamba, hivi sasa hajulikani mahali aliko na Polisi inaendelea na uchunguzi na endapo atakamatwa hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Katika hatua nyingine jeshi hilo la Polisi mkoani humo, limemtia mbaroni Abdallah Juma mkazi wa Mjimwema katika Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kukutwa na gramu 500 za bangi alizokuwa amezihifadhi kwenye mfuko wa rambo.

Tukio hilo lilitokea Machi 28 mwaka huu, majira ya saa 5:40 asubuhi huko katika maeneo ya Matarawe mjini hapa. 

Mtuhumiwa Juma alikamatwa na askari Polisi, ambao walikuwa doria  kwenye eneo hilo la Matarawe katika kibanda alichokuwa akifanyia biashara ya kuuzia bangi, ambapo muda wowote kuanzia sasa mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

No comments: