Friday, April 1, 2016

WANANCHI TUNDURU WAPATIWA HUDUMA YA MATIBABU MACHO BURE

Na Steven Augustino,
Tunduru.

ZAIDI ya watu 5,000 waishio wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamenufaika na huduma ya matibabu ya macho iliyotolewa wilayani humo kwa lengo la kuboresha afya zao, kutokana na wengi wao kusumbuliwa na matatizo mbalimbali ya magonjwa ya macho.

Shirika la Bilal Musilm Mission, ndilo lililotoa huduma hiyo ambapo Dkt. Ain Sharif ambaye ni mratibu wa huduma hiyo alisema kuwa ilikuwa ikitolewa hivi karibuni katika shule ya  sekondari, Frank Weston iliyopo mjini hapa.

Sharif alisema kuwa jumla ya madaktari 12 wakiwemo madaktari bingwa watano wa huduma za macho walishiriki katika zoezi hilo, ambalo lilidumu kwa muda wa siku nne.

Alisema wataalamu hao walitoa huduma ya kupima macho, kutoa dawa, kufanya upasuaji wa kutoa mtoto wa jicho na kutoa miwani kwa watu waliobainika kuwa na mahitaji hayo.

Kwa mujibu wa Dkt. Sharif pamoja huduma hizo kutolewa, pia shirika hilo ambalo liliambatana na madaktari hao na kundi kubwa la wafanyakazi wa kujitolea walifanya upasuaji kwa watu zaidi ya 300, ambao walikuwa wakisumbuliwa na matatizo ya mtoto wa jicho.

Alisema katika utekelezaji wa zoezi hilo, walitoa huduma hiyo pamoja na waliohitaji kupatiwa dawa za kutibu matatizo ya macho yao, huku huduma hizo zikitolewa bure bila malipo yoyote.

Ni mwaka wa 27 mfululizo kwa shirika hilo kutoa huduma hizo,  katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dkt. Mmari Zabron pamoja na kuwapongeza viongozi wa shirika hilo kwa uamuzi wa kupeleka huduma hiyo wilayani humo, aliwataka wananchi wenye matatizo mbalimbali ya kiafya kuendelea kujitokeza kwa wingi ili waweze kupatiwa huduma.

Alisema wilaya hiyo ina uhitaji mkubwa wa huduma za macho na kwamba watu wengi wamekuwa wakiishi katika upofu, kutokana na kushindwa kumudu gharama zake ambazo hutolewa katika hospitali za kulipia.

Wilaya ya Tunduru ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na magonjwa ambayo husababisha upofu yakiwemo usubi na trachoma.

No comments: