Thursday, April 7, 2016

MILONJI LUSEWA WATAKIWA KUPELEKA WATOTO WAO SHULE



Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Milonji,  kata ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wameaswa kupeleka kwa wingi watoto wao shule  ili waweze kupata elimu, ambayo itawasaidia kutoka katika hali  ya umaskini unaowakabili kwenye familia zao.

Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wazazi na walezi  pamoja na wananchi  wa kijiji hicho, katika mkutano wa hadhara wenye lengo la kutafuta majawabu  ya kukabiliana na changamoto zilizopo za watu kutotaka kupeleka watoto wao shule, alipokuwa kwenye ziara ya siku mbili katika kata ya Lusewa wilayani humo.
Chande Nalicho.

Alisema kuwa, baadhi ya wazazi wamekuwa hawatendi haki kwa watoto wao kwa kuwapa mahitaji ya msingi ikiwemo suala la kuwapatia elimu, jambo ambalo ni sawa na ukatili mkubwa unaofanywa na wazazi  kwa watoto wao.

Alisisitiza kuwa kila mzazi anaowajibu wa kuhakikisha watoto alionao watakapofikisha umri wa  kwenda shule, ni lazima wawe wameripoti shule ili wapate elimu ambayo ni urithi  endelevu katika maisha yao ya kila siku.

Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo alifafanua kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita,  tayari  shule ya msingi Milonji imekwisha andikisha watoto 107  na imekuwa shule ya 8 ambayo inaongoza kwa kuitikia wito wa Rais Dkt. John Magufuli ya elimu bure.


Katika hatua nyingine amewataka wananchi kushikiriana na serikali, katika kupunguza tatizo kubwa la uhaba wa madawati linaloikabili shule hiyo kwani mpaka sasa mahitaji halisi ni madawati 117, kwa hiyo watumie rasilimali za misitu zilizopo katika maeneo yao kukabiliana na upungufu huo mkubwa wa madawati.

Katika mpango huo, sio kila jambo lazima lifanywe na serikali yao bali kila mmoja anapaswa kuhakikisha kwamba ni sehemu ya mafanikio katika mpango huo ambao utasaidia, kuongeza kiwango cha ufaulu kwa vijana wao.

No comments: