Thursday, April 21, 2016

WANANCHI WAITAKA HALMASHAURI KUWAUNGA MKONO



Na Kassian Nyandindi,
Njombe.

WAKAZI wa kijiji cha Mwilamba kata ya Kipengele wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, wameitaka Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi hao, juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji vilivyopo kijijini hapo ambavyo ni tegemeo kubwa kwa mkoa huo.

Aidha wamemuomba Mkuu wa wilaya hiyo, Asumpta Mshama kuacha kutumia muda mwingi kukaa ofisini badala yake atembelee vyanzo hivyo ambapo walieleza kuwa serikali ya wilaya, imevitelekeza kwa miaka mingi na kuwaachia wananchi pekee waendelee kuvitunza.

Kauli hiyo ilitolewa na wakazi hao ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini, walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kijijini hapo, kwa ajili ya kujionea changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.


Wakizungumzia juu ya vyanzo hivyo, walisema kuwa kijiji hicho kina zaidi ya vyanzo vya maji 26 ambavyo ndiyo huzalisha maji na kutumika katika maeneo ya Njombe hivyo wanashangazwa na uongozi wa wilaya hiyo, kukaa kimya bila kutembelea wananchi hao na kuunga mkono jitihada wanazozifanya katika kuendelea kuimarisha vyanzo hivyo.

“Sisi wakazi wa kijiji hiki ndio tunaofanya kazi ya kutunza vyanzo hivi, mara kwa mara tunapanda miti rafiki ya maji kwa lengo la kuimarisha uoto wa asili usiweze kupotea, tumepeleka taarifa huko wilayani ili wataalamu waweze kufika hapa kijijini kwetu watupatie elimu ya utunzaji wa mazingira hatuja waona kwa muda mrefu na hii inaonesha kwamba hawataki kutekeleza jambo hili”, walisema.

Lukemelo Mgaya ambaye ni diwani wa kata ya Kipengele, alipohojiwa na waandishi wa habari alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo na kueleza kwamba jambo hilo alilifikisha kwa viongozi husika ili liweze kufanyiwa kazi, lakini anashangaa kuona hakuna utekelezaji uliofanyika.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Meckedezeki Humbe alipoulizwa kuhusiana na kero hiyo alisema ofisi yake haijawahi kupokea malalamiko hayo ya utunzaji wa vyanzo vya maji kwa wananchi wa kijiji cha Mwilamba.
“Jambo hili kwangu ni jipya ndio kwanza mnaniambia, mimi sijasikia lolote juu ya malalamiko haya subirini nikalifanyie kazi”, alisema Humbe.

Mkuu wa wilaya hiyo, Asumta Mshama alipotakiwa kutolea ufafanuzi kwamba pamoja na ofisi yake kuwa na taarifa juu ya suala hilo alisema yeye hajawahi kupokea kero yoyote ya vyanzo hivyo, huku akiongeza kuwa mnamo Machi 3 mwaka huu alitembelea kijiji hicho na wananchi hawakumwambia jambo lolote lile kuhusiana na malalamiko hayo.

No comments: