Saturday, April 16, 2016

DIWANI AJIKUTA AKIINGIA KATIKA KASHFA NZITO NA FEDHA ZA TASAF



Na Steven Augustino,
Tunduru.

DIWANI wa kata ya Tuwemacho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, Khadija Mohamed amejikuta akiingia katika kashfa nzito baada ya kubainika alikuwa amejiandikisha miongoni mwa kaya maskini, ambazo zimeingizwa kwenye mradi wa uhaulishaji fedha unaotekelezwa na Mfuko wa Mendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani humo.

Khadija alibainika kuingizwa kwenye mpango huo, huku akitambua kwamba anao uwezo wa kujimudu kimaisha, ambapo alibainika kufanya hivyo baada ya TASAF wilayani hapa kufanya zoezi la kuhakiki majina ya walengwa wanaostahili kupewa msaada wa fedha hizo ambao ni maskini hawajiwezi.

Sambamba na diwani huyo pia zoezi hilo limemng'oa Kaimu mtendaji wa kijiji cha Nasya katika kata hiyo, Msamati Omary ambaye naye alijiandikisha kuwa ni kati ya watu ambao wanastahili kupewa fedha hizo.


Kufuatia hali hiyo wengine walioondolewa katika mpango huo, ni pamoja na Mwenyekiti wa kitongoji cha Malolo, aliyefahamika kwa jina la Mohamed Malolo.

Pia Mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Mohamed Milanzi naye alikumbwa na kadhia hiyo wakati zoezi hilo linafanyika.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo, Mshauri na mfuatiliaji wa miradi  ya Mfuko wa maendeleo ya jamii wilaya ya Tunduru Christian Amani, alisema wanufaika hao wameondolewa baada ya uchunguzi uliofanyika na kubaini hawana sifa za uwepo wao katika mpango huo kwa sababu wanajiweza katika kumudu maisha yao ya kila siku.

“Tumefanya hivi kwa lengo la kuhakiki na kuwaondoa wajanja wachache waliojipenyeza kiujanja ujanja katika mradi huu, ili wapate fedha za kufanyia starehe za maisha yao”, alisema Amani.

Alisema inonesha kwamba, viongozi hao walijipenyeza kwa kutumia mlango wa nyuma na wananchi wakawa wanashindwa kuwataja kwa kuwaogopa huku akiwataka kutokana na kuenguliwa huko, waandike barua za kukata rufaa na kuzipeleka TASAF ili zijadiliwe upya na kuzipitia kwa ajili ya kuondoa utata endapo itabainika kama wameonewa.

Vilevile Amani alifafanua kuwa baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, utafanyika utaratibu mpya wa kuingiza kaya zinazostahili kulingana na sifa zilizoainishwa na mfuko huo ili kuweza kuepukana na matatizo kama hayo yanayoweza kujitokeza tena hapo baadaye. 

No comments: