Saturday, April 16, 2016

WAJASIRIAMALI MANISPAA SONGEA WAIANGUKIA SERIKALI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANAWAKE ambao ni wajasiriamali katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameiomba serikali kuwaandalia maeneo maalum ya kufanyia shughuli zao za kila siku ili waweze kujiingizia kipato, badala ya kutumia maeneo yasiokuwa rasmi ambayo yamekuwa yakiwasababishia adha kubwa wakati wanapofanya biashara zao.

Baadhi ya wanawake hao walisema hayo hivi karibuni, walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi huku wakieleza kuwa licha ya kujikita na kutumia zaidi nguvu kubwa katika shughuli zao, changamoto kubwa wanayokabiliana nayo hivi sasa ni kukosekana kwa mazingira rafiki ya kufanyia shuguli zao badala yake hulazimika kutumia maeneo ambayo hayajatengwa kisheria jambo ambalo huwasababishia usumbufu mkubwa, wa kufukuzwa na askari mgambo wa Manispaa hiyo.

Walisema kuwa, jambo hilo linawafanya kushindwa kusonga mbele kimaendeleo katika maisha yao ya kila siku na hata  kushiriki wakati wa kuchangia  shughuli mbalimbali za kijamii.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wajasirimali hao Mary Mapunda anayejishughulisha na biashara ya kuuza matunda  kando kando ya soko kuu la Manispaa ya Songea, alisema kuwa licha ya Manispaa kuwaruhusu kufunga baadhi ya barabara ili kupisha shughuli zao ziweze kufanyika, hata hivyo bado maeneo hayo sio  salama kwao kutokana na muda mchache wanaopewa kufanya shughuli hizo za kibiashara.

Kwa mujibu wa Mapunda alifafanua kuwa muda wanaopewa ambao ni  kuanzia saa 12 jioni na kuendelea sio muda sahihi kwao, kwa sababu wateja wengi tayari wanakuwa wamesharudi nyumbani na wanakuwa wamekwisha nunua mahitaji yote ya nyumbani.

Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za  kuuza matunda, kama vile ndizi, embe na mbogamboga lakini pindi wanapotafutwa na wateja wao hawapatikani kutokana na kukosekana kwa eneo maalum, ambalo lingewakutanisha wajasirimali wanaouza bidhaa hizo kwa wateja wao.

No comments: