Tuesday, April 26, 2016

BONANZA LA VIJANA MBINGA LASISITIZA MASUALA YA USAFI WA MAZINGIRA PIA LATOA MSAADA WA VIFAA MBALIMBALI KWA WATOTO YATIMA

Baadhi ya wanabonanza la vijana wa Mbinga mkoani Ruvuma, la kuelimisha rika na usafi wa mazingira wakishiriki kuzoa taka katika eneo la soko la wakulima Mbinga mjini.

Wanabonanza wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga mara baada ya kuwasili katika kituo cha Twiga kilichopo mjini hapa ambacho hulea watoto Yatima wanaoishi katika mazingira magumu.

Upande wa kulia Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Senyi Ngaga akikabidhi mafuta ya kupikia na vitu vingine mbalimbali kwa mlezi wa kituo cha kulea watoto Yatima ambao wanaishi katika mazingira magumu kinachofahamika kwa jina la Twiga, kilichopo Mbinga mjini. Msaada huo ulitolewa na Bonanza la vijana wa Mbinga la kuelimisha rika na usafi wa mazingira.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI waishio katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia masuala ya usafi kuanzia kwenye mazingira yao wanayoishi majumbani kwao hadi katika maeneo wanayofanyia kazi au biashara, ili waweze kuuweka mji huo katika hali ya usafi na kuepukana na magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alipokuwa kwenye maadhimisho ya bonanza la vijana wa Mbinga la kuelimisha rika na usafi wa mazingira, lililofanyika juzi katika uwanja wa taifa mjini hapa.

Bonaza hilo lilikuwa likienda sambamba na kauli mbiu isemayo; zuia ngono zembe, mimba za utotoni, madawa ya kulevya na elimu inalipa.

Maadhimisho hayo yalifanyika kwa kuanza kufanya usafi katika eneo la soko la wakulima lililopo mjini hapa kwa kuwashirikisha wananchi, watumishi wa serikali na wale wanaotoka kwenye sekta binafsi.

Watoto Yatima wakiwa na Wanabonanza kituo cha Twiga Mbinga.
Aidha waliweza kuwatembelea watoto yatima ambao wanalelewa katika kituo cha kulea watoto hao wanaoishi katika mazingira magumu kinachofahamika kwa jina la Twiga, kilichopo kata ya Matarawe Mbinga mjini kwa kuwapatia msaada wa vitu mbalimbali kama vile sabuni za kuogea na kufulia, daftari, kalamu, mafuta ya kupikia, sukari, pamoja na sare za shule.

Ngaga alisema kuwa kuna kila sababu katika jamii kuona umuhimu wa kusaidia watoto hao, ili wasiweze kujiona wakiwa katika hali ya kutengwa kwa kuwasomesha na hatimaye waweze kutimiza ndoto yao ya kuwa na maisha bora.


Awali akitolea ufafanuzi juu ya maadhimisho hayo, Katibu wa bonanza hilo Charles Kilili aliwaeleza waandishi wa habari kuwa msukumo wao kama vijana ni kupeleka elimu kwa jamii, hasa kwa watoto wa kike waweze kuepukana na mimba za utotoni na kwa wale wa kiume waachane na uvutaji wa madawa ya kulevya kama vile bangi.

“Tunafanya haya mambo kwa kusisitiza masuala ya elimu husika iweze kuwafikia kwa vitendo, tutahamasisha jamii uanzishaji na uundaji wa klabu za kuelimisha watoto mashuleni juu ya kuachana na vitendo hivi, lengo ni kuwapa elimu ya makuzi ikiwemo masuala ya uzazi wa mapango”, alisema Kilili.

Kilili alifafanua kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wametimiza azma yao ya kuwataka wanafunzi waepukane na hali hiyo kwa kujifunza juu ya matendo mema wanayopaswa kuyafuata ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao darasani na kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Naye Baraka Mwabulesi ambaye ni Mwenyekiti aliyekuwa akiongoza maadhimisho ya bonanza hilo la uelimishaji rika na usafi wa mazingira, alisema kwa upande wa kuweka mazingira wakati wote katika hali ya usafi wanafanya hivyo kwa lengo la kuhamasisha jamii, kuwa na mazoea ya kufanya usafi mara kwa mara katika maeneo yao.

Baraka alieleza kuwa jambo hilo wamelifanya kwa kumshirikisha pia afisa afya wa halmashauri ya mji wa Mbinga, ili liweze kuwa endelevu kwa wananchi wote wanaoishi katika mji huo.

Pamoja na mambo mengine wanabonanza walitoa vifaa vya kufanyia usafi ambavyo ni vifaa vya kuhifadhia taka (dust bin), mifagio ya kisasa, sabuni na ndoo za kunawia maji mara baada ya kufanya usafi, ambavyo vilikabidhiwa kwa wafanyabiashara wa soko la wakulima lililopo mjini hapa.

No comments: