Monday, July 24, 2017

DED MADABA AWAASA WAZAZI KUZINGATIA UZAZI WA MPANGO

Na Muhidin Amri, 
Madaba.

WAZAZI na walezi  katika Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, wameaswa kutambua wajibu wa malezi kwa watoto wao ikiwemo  kuzingatia uzazi wa mpango, ili kuweza kuepuka kuwa na idadi ya watoto wengi katika familia zao ambao ni mzigo mkubwa kutokana na hivi sasa kupanda kwa gharama ya maisha.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa endapo watazingatia ipasavyo itawezesha watoto watakaozaliwa kupata haki yao ya msingi kama vile elimu, chakula, mavazi na kumudu gharama ya matibabu jambo ambalo litachangia kuwa na familia bora na yenye afya nzuri.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani humo, Shafi Mpenda alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wazazi na walezi katika kituo cha afya Madaba ambao walikuwa kituoni hapo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za matibabu.


Alisema kuwa baadhi ya wazazi hawana utaratibu na mazoea ya kuchagua idadi ya watoto wa kuzaa ambao wataweza kumudu gharama za malezi yao na badala yake kutokana na tamaa za mwili hujikuta wakiwa na idadi kubwa ya watoto ambapo baadaye hushindwa kuwapatia huduma muhimu hivyo kuongezeka kwa idadi kubwa ya watoto katika familia na huishia kuzurula mitaani.

Mpenda alieleza kuwa ni vizuri sasa wakati umefika kwa Watanzania hususan kwa wakazi wa Madaba kuchagua idadi ya  watoto wa kuzaa kwa kupanga aina ya maisha unayotaka badala ya kuishi maisha ya ufahari na sifa jambo ambalo linachangia kurudisha nyuma maisha na ndoto ya kuwa na maendeleo.

Aliongeza kuwa kutokana na aina ya maisha wanayoishi baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo ya Madaba ni vigumu pia kupata hata viongozi bora kwani hata wale waliopo huko vyuoni ambao wanategemewa kuwa viongozi wa kesho tayari wameanza kujiingiza katika vitendo vya mambo ya anasa ambavyo kwa kiasi kikubwa yamekuwa hayaendani na maadili na tamaduni zao.

“Ni jambo la kusikitisha kuona idadi kubwa ya wasichana kuanzia miaka 16 hadi 18 wanapata ujauzito mapema wakiwa bado shuleni, mimba katika kundi hili zinazidi kuongezeka kila kukicha huku wazazi na jamii ikiendelea kufumbia macho vitendo hivi bila kuchukua hatua juu ya namna ya kudhibiti”, alisema.


Kwa mujibu wa Mpenda alisema kutokana na tatizo hilo kuwa sugu ndiyo maana idadi ya vitendo vya kutupa watoto pindi wanapozaliwa vinazidi navyo kushamiri siku hadi siku huku akiiomba jamii kushirikiana na vyombo husika kama idara ya ustawi wa jamii na Polisi kupambana navyo kwa kuwabana watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani vimekuwa vikiliaibisha taifa.

No comments: