Monday, July 10, 2017

MGOGORO WA WAKULIMA ULIODUMU KWA MUDA MREFU MADABA WAMALIZWA

Na Mwandishi wetu,     
Madaba.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma Shafi Mpenda amefanikiwa kumaliza mgogoro uliodumu kwa muda mrefu, kati ya wakulima wanaozalisha mahindi na uongozi wa serikali ya kijiji cha Madaba wilayani humo ambao walikuwa wakigombea umiliki wa ghala la kuhifadhia mahindi lililopo kijijini humo.

Mgogoro huo ambao umedumu kwa muda wa miaka miwili, ukihusisha pande mbili kati ya wakulima hao kupitia kikundi chao cha KIWAMA ulisababisha wakulima kutokuwa na sehemu ya kuhifadhia mahindi yao katika kipindi cha mavuno baada ya ghala hilo kutumiwa na Wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula.

Alisema kuwa ghala hilo limejengwa na serikali kwa gharama ya shilingi milioni 85 kupitia halmashauri ya wilaya ya Songea kabla ya kugawanywa na kuzaliwa halmashauri mpya ya wilaya ya Madaba, ili liweze kuwasaidia wakulima hao kupitia vikundi vyao vya kukusanyia mazao ya chakula na biashara hasa mahindi wakati wanapokuwa wakisubiri soko la kuyauza.
 

Mpenda ameuagiza uongozi wa kijiji cha Madaba kuweka utaratibu maalum wa kutumia ghala hilo ili kila upande uweze kulitumia badala ya kunufaisha upande mmoja.

Hali kadhalika aliongeza kwa kuwataka viongozi wa vijiji na kata ndani ya wilaya hiyo, kuhakikisha kwamba wanahimiza wananchi wao kufanya shughuli za kimaendeleo kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


Selina Kilumile ambaye ni Mweka  hazina wa kikundi cha KIWAMA alisema kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 kikundi hicho kimeweza kuzalisha ekari 991 za zao la mahindi, lakini changamoto kubwa inayowasumbua hivi sasa ni sehemu ya kuhifadhi mazao hayo pamoja na soko la kwenda kuyauza ili waweze kupata fedha za kuendeshea maisha yao.

No comments: