Thursday, July 20, 2017

KATIBU MKUU CHADEMA NA WENZAKE WAPANDISHWA KIZIMBANI SONGEA

Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwa katika Mahakama ya mkoa wa Ruvuma jana, ambapo wamesomewa mashtaka mawili na kupelekwa Mahabusu ya gereza Songea mjini.
Na Muhidin Amri,     
Songea.

VIONGOZI tisa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Katibu Mkuu wa chama hicho  Dokta Vicent Mashinji wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu mkazi mfawidhi mkoa wa Ruvuma, kujibu mashtaka mawili yanayowakabili na baadaye wamepelekwa  katika gereza la Mahabusu Songea mjini huku kukiwa kumegubikwa na hali ya utata.

Aidha viongozi hao wamefikishwa Mahakamani hapo jana majira ya asubuhi na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa serikali mwandamizi mkoani hapa, Renatus Mkude  ambaye alikuwa akisaidiwa na Wakili wa serikali Shaban Mwigole mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama ya mkoa huo, Simon Kobelo.

Wakili Mkude aliwataja Mahakamani hapo washitakiwa hao kuwa ni Dokta Vicent Mashinji ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA taifa, Cecil Mwambe Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya kusini ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ndanda Mtwara, Philberth Ngatunga Katibu wa CHADEMA Kanda ya kusini, Irineus Ngwatura Mwenyekiti CHADEMA mkoa wa Ruvuma pamoja na Delphin Gazia Katibu wa CHADEMA mkoa wa Ruvuma.

Wengine ni Zubeda Sakuru  Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Ruvuma, Sanguru Manawa Katibu wa Oganaizesheni na mafunzo, Curthberth Ngwata Mwenyekiti CHADEMA wilaya ya Nyasa ambaye pia ni Diwani wa kata ya Kipingu wilayani humo pamoja na Charles Makunguru Katibu mwenezi wilaya ya Nyasa.


Mkude alidai Mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na makosa mawili ambayo ni kosa la kwanza wote kwa pamoja wakiwa wilayani Nyasa tarehe isiyofahamika walikula njama ya kutenda kosa ambalo lingeweza kusababisha uvunjifu wa amani ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alilitaja kosa la pili kwamba wanadaiwa kuwa mnamo Julai 15 mwaka huu katika eneo la mji wa Mbambabay washitakiwa wote kwa pamoja walifanya mkusanyiko usio wa halali ambao ungepelekea kusababisha uvunjifu wa amani katika jamii.

Vilevile aliiambia mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa na kwamba washtakiwa wote wamekana mashitaka yote mawili na wamerudishwa mahabusu katika gereza la Songea mjini.

Kwa upande wake Hakimu Kobelo alisema kuwa dhamana ya washitakiwa ipo wazi hivyo kila mshtakiwa anapaswa kuwa na wadhamini ambao ni wakazi wa Songea mjini ambao wanatakiwa wapeleke uthibitisho toka kwa Maafisa watendaji wa mitaa wanayoishi mjini hapa, pia wadhamini hao wanatakiwa kudhaminiwa kwa shilingi milioni mbili ya maneno.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 20 mwaka huu  itakapokuja kwa ajili ya kutajwa tena ambapo pia mara baada ya Mahakama hiyo kuahirisha kesi  hiyo na kuwataka mawakili wa upande wa utetezi ambao ni Edson Mbogoro, Eliseus  Ndunguru  wote wa  Songea pamoja na mawakili wasomi waandamizi Barnabas Pomboma toka Mbeya.

WAkati mawakili hao wakishughulikia masuala ya dhamana za wateja wao Hakimu huyo alitoka na kudaiwa amekwenda Mahakama kuu kanda ya Songea ambapo mawakili hao walimsubiri kwa muda mrefu na alipofika ilionekana wakili wa serikali naye alitoka huku akiaga anatoka kwa muda na atarejea ili aweze kusaini hati hizo za dhamana, lakini hakuweza kutokea na baada ya kupigiwa simu yake ya mkononi ilikuwa imezimwa hakuweza kupatikana.

Kwa upande wake wakili msomi Edson Mbogoro aliwaeleza  waandishi wa habari kuwa viongozi hao wamefunguliwa kesi ya Jinai namba 173 ya  mwaka 2017  wao walikwenda kumuona Hakimu ili aweze kuthibitisha dhamana za wateja wake lakini cha ajabu hadi muda wa kazi wa Mahakama unakwisha Hakimu hakuweza kutokea mahakamani hapo hivyo wanasubiri kesho waweze kuzungumza na  Hakimu huyo ili awaeleze nani aliyetoa hati ya wateja wao kupelekwa mahabusu.

Pia Mbogoro alilalamikia kitendo cha watu 12 tu kuruhusiwa kuingia mahakamani na wengine kuzuiwa ambao walikuja mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Naye Wakili msomi Eliseus Nduguru amelalamikia wateja wake kutoroshwa katika mazingira ya kutatanisha na kupelekwa mahabusu bila kufuata taratibu ambapo hakuweza kuyaelewa mazingira hayo waliyoyafanya walikuwa na nia gani kwani yeye na mawakili wenzake walikuwa wakishugulikia dhamana ambapo alisema kuwa kuna mchezo mchafu ambao ukiendelea kuachwa ipo siku utaweza kuleta madhara kwa wengine.


Hata hivyo Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana taifa (BAVICHA ) Patrick Ole Sosopi ameitaka Mahakama kutenda haki  na siyo kufanya mambo tofauti na sheria inavyotaka, pia Jeshi la Polisi lifanye kazi kwa weledi na pia limeonyesha wazi kuvunja sheria  za nchi tangu mwanzo kwa sababu waliwazuia wananchi wengine waliofika Mahakamani kusikiliza kesi hiyo pale walipotaka kuingia ndani ya Mahakama na badala yake waliruhusiwa watu 12 tu.

No comments: