Thursday, July 27, 2017

WANANCHI MBINGA WASIKITISHWA KITENDO CHA SERIKALI KUHAMISHA WATUMISHI WAKE KADA YA AFYA

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesikitishwa na kitendo cha serikali kuchukua hatua ya kuhamisha watumishi wake wa kada ya afya ambao walikuwa wakitoa huduma kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizokuwa chini ya mamlaka ya Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani humo.
Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto, Ummy Mwalimu.

Aidha wameiomba serikali kuwarejesha watumishi hao katika maeneo waliyokuwa wakifanyia kazi kwenye Jimbo hilo, ili kuweza kunusuru hali za wagonjwa waliokuwa wakipatiwa matibabu katika vituo hivyo vya kutolea huduma za afya.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari walisema kuwa hivi sasa uongozi wa Jimbo Katoliki la Mbinga unashindwa kuendelea kutoa huduma za afya katika vituo hivyo kutokana na kukosa wauguzi na wataalamu wenye uwezo wa kutibu wagonjwa.

Pia walidai kuwa kufuatia hali hiyo hospitali ya misheni Litembo na vituo vingine vinavyoendeshwa na Jimbo hilo muda wowote kuanzia sasa huenda vikafungwa visitoe huduma kwa wagonjwa kutokana na kukosa watumishi wenye uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali.

Vilevile akizungumza kwa niaba ya wananchi wenzake, Aidan Challe ambaye ni mkazi wa kijiji cha Myangayanga kata ya Myangayanga wilayani hapa alisema kuwa kutokuendelea na utiaji wa saini kwa mikataba mipya ya ubia baina ya serikali na vituo vya kutolea huduma vya binafsi ni sawa na kuumiza wananchi, kwani ndani ya wilaya ya Mbinga tegemeo kubwa la watu kupatiwa matibabu ya uhakika yapo katika hospitali hiyo ya Misheni Litembo.

Challe alisema vituo vya serikali vya kutolea huduma za afya vilivyopo wilayani humo vingi vimekuwa havitoi huduma bora kutokana na kuwa na upungufu wa madawa na vifaa tiba vya kutibu wagonjwa hivyo watu wengi wamekuwa wakikimbilia kwenye vituo vya Jimbo Katoliki la Mbinga kupatiwa matibabu kutokana na huduma zao kuwa bora.

“Tunaiomba serikali iangalie upya namna ya kurejesha mikataba hii ya ubia na hawa wenzetu wa Jimbo hili, leo vituo vyao vya kutolea huduma za afya kama vile hospitali hii ya Litembo ambayo ndiyo tegemeo kubwa kwa wilaya yetu jimbo linataka kuifunga kutokana na agizo hili lililotolewa la kuwahamisha watumishi wake mimi binafsi nahoji je tutakimbilia wapi kuokoa uhai wetu pale tutakapougua?”, alisema Challe.

Kadhalika naye Joackimu Kinemela ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mapera kata ya Maguu alisema kuwa uamuzi huo uliochukuliwa na serikali unapaswa kuangaliwa upya kwani kwa kiasi kikubwa ni sawa na kuwapa mateso wananchi ambao hawana hatia mbele ya Mungu.

Mratibu wa afya Jimbo hilo la Mbinga, Padri Raphael Ndunguru naye aliwaeleza waandishi wa habari kuwa wapo katika hatua ya kuvifunga vituo vyao vya kutolea huduma za afya kutokana na kuwa na upungufu mkubwa wa watumishi wenye sifa ya kuhudumia wagonjwa.

Padri Ndunguru aliongeza kuwa uongozi wa jimbo unatambua kwamba kitendo hicho kilichofanywa na serikali kuwahamisha watumishi wake watakaoathirika kwa kiasi kikubwa katika tukio hili ni wananchi hivyo kuna umuhimu wa kukaa na kujadili suala hilo kwa pamoja kati ya serikali na jimbo ili kuweza kufikia muafaka mzuri juu ya jambo hilo.

“Sisi hatuoni kama kuna sababu ya msingi ya kuwahamisha watumishi hawa, tumeishi nao vizuri kwa miaka mingi na kufanya nao kazi pamoja hivyo tunaiomba serikali iturejeshee tena watumishi hawa ili tuweze kuendelea kuhudumia wananchi wetu”, alisema Padri Ndunguru.

Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko alipoulizwa juu ya watumishi wa serikali kutokuendelea utiaji wa saini kwa mikataba mipya ya ubia na vituo vya kutolea huduma binafsi alikiri kuwepo kwa jambo hilo huku akikataa kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo licha ya ofisi yake ndiyo iliyohusika kutoa maagizo hayo ya kuhamisha watumishi hao.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu unathibitisha kuwa agizo hilo lilitolewa na ofisi ya Katibu tawala huyo kupitia barua ya Aprili 18 mwaka huu ambayo nakala yake tunayo, yenye kumbukumbu namba EC. 124/138/01/A/31 kwenda kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya hapa mkoani Ruvuma kwa ajili ya utekelezaji wa suala hilo.

No comments: