Tuesday, July 18, 2017

KATIBU MKUU CHADEMA TAIFA NA WENZAKE KUFIKISHWA MAHAKAMANI SONGEA KESHO

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

VIONGOZI nane wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Katibu Mkuu taifa wa chama hicho, Dokta Vicent Mashinji wameripoti kwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma jana majira saa nne asubuhi na wapo nje kwa dhamana wakisubiri hatma yao.

Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gemini Mushy alisema kuwa viongozi hao waliripoti Ofisini kwake majira hayo ambapo alikuwa akisubiri Jalada la kesi yao ambalo lipo kwa Wakili wa serikali mfawidhi mkoa wa Ruvuma.

Aliwataja viongozi hao wanaotuhumiwa kuandamana na kufanya mkutano bila kibali katika wilaya ya Nyasa kuwa ni Cecil Mwambe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya kusini na Mbunge wa jimbo la Ndada, Philbert Ngatunga Katibu wa Kanda ya kusini CHADEMA, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Ruvuma Ereneus Ngwatura na Delphin Gazia ambaye ni Katibu wa chama hicho mkoa wa Ruvuma.


Wengine ni Zubeda Sakuru Mbunge Viti maalum mkoa wa Ruvuma kupitia tiketi ya chama hicho, Sang’uda Moses Mkuu wa Organization na mafunzo CHADEMA, Carthberth Ngwata Mwenyekiti wilaya ya Nyasa wa chama hicho pamoja na Charles Makunguru Katibu mwenezi wilaya ya Nyasa.

Kadhalika Kamanda Mushy aliwataka wanachama na wapenzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kuwa watulivu wasivunje sheria, bali waendelee kuwa watulivu.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa Chama hicho Dokta Mashinji akizungumza na mwandishi wetu nje ya Ofisi za CHADEMA mkoani Ruvuma zilizopo katika mtaa wa Matarawe Manispaa ya Songea, alisema kuwa walikamatwa na kuambiwa wamevunja sheria kwa kufanya maandamano na mkutano jambo ambalo halikuwa la kweli kwani wao walikwenda Mbambabay kwa kutaka kufanya kikao cha ndani ambapo walipotaka kuanza ndipo waliposhitukia kuona askari wakiwazunguka na kuwakamata.

“Hii inaonyesha ni mikakati ya wazi na ya makusudi kuwavuruga wanachama wetu ili wasifanye maendeleo yao ndani ya chama chetu wakati Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kufanya mikutano ya ndani na wala hakisumbuliwi”, alisema Mashinji.

Aliiomba serikali ione umuhimu wa kujali siasa za mfumo wa vyama vingi na siyo kuwawekea vikwazo pale wanapojaribu kujipanga kwa ajili ya chaguzi zijazo huku akiongeza kwa kuwataka wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo kote nchini waendelee na shughuli za chama kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo na wasiogope mtu yeyote.

Hata hivyo hadi kufikia leo viongozi hao wapo nje kwa dhamana wakisubiri taratibu zingine za kufikishwa kesho Mahakamani.

No comments: