Monday, July 17, 2017

MADABA WANANCHI WAKE KUNUFAIKA NA MRADI WA NISHATI YA UMEME

Na Muhidin Amri,          
Madaba.

WANANCHI wanaoishi katika vijiji vilivyopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, wanatarajia kuanza kunufaika na mradi wa nishati ya umeme ambao utasambazwa katika maeneo mbalimbali wilayani humo.

Mradi huo unatarajiwa kuanza mapema mwezi Agosti mwaka huu, ambapo serikali imepeleka Jenereta kubwa ambalo litajengwa kwa ajili ya kusambaza nishati hiyo muhimu.

Aidha mbali na kuusambaza kwenye vijiji hivyo, pia utapelekwa makao makuu ya Ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kusaidia kuimarisha mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya Kielektroniki.


Shafi Mpenda ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba alisema hayo kuwa Jenereta hilo limetolewa ikiwa ni sehemu ya ahadi ya Rais Dokta John Magufuli ya kupeleka nishati ya umeme nchi nzima kwa ajili ya kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Mpenda aliongeza kwa kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya maandalizi ya kuupokea umeme huo kwa kujenga miundombinu husika kwenye nyumba zao ili waweze kuunganishiwa nishati hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo ni kwamba dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ni kutaka kuona umeme huo unatumika kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa ili kukuza na kuharakisha ukuaji wa maendeleo ya wananchi wake.


Pia umeme huo utawasaidia wananchi wa Madaba kuweza kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika matunda kutokana na hivi sasa wengi wao huzalisha matunda mengi na huishia kuoza kutokana na kutokuwepo kwa viwanda hivyo kwa ajili ya usindikaji.

No comments: