Sunday, July 30, 2017

WAMILIKI WA VIWANDA WATAKIWA KUWATUMIA VIJANA WANAOMALIZA MAFUNZO VETA

Na Muhidin Amri,      
Songea.

WITO umetolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri mkuu, sera, bunge, ajira, vijana na watu wenye ulemavu Jenista Mhagama kwamba wamiliki wa viwanda pamoja na taasisi mbalimbali hapa nchini wajenge ushirikiano na vijana wanaomaliza mafunzo katika vyuo vya mafunzo na ufundi stadi (VETA) hapa nchini, kwa ajili ya kuzalisha bidhaa zitakazotosheleza mahitaji ya ndani na nje ya nchi ili kuweza kufikia uchumi wa kati.

Alisema kuwa kufanya hivyo ni hatua ambayo itasaidia kuwa na bidhaa zinazoweza kutosheleza mahitaji ya soko la ndani badala ya kukimbilia kutafuta nguvu kazi na bidhaa zinazotoka nje ya nchi.

Waziri Mhagama alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na  wanafunzi, walimu wa chuo cha VETA Songea pamoja na vijana 173 kutoka wilaya za mkoa wa Ruvuma, kwenye uzinduzi wa mpango  wa urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo katika chuo hicho cha mafunzo ya ufundi stadi kilichopo mjini hapa.


Alieleza kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati, ifikapo mwaka 2025 ambao ni mwelekeo wa miaka mitano kuanzia 2016 hadi 2021 wenye lengo la kujenga Taifa lenye viwanda vingi vya uzalishaji  bidhaa na kuuza nje ya nchi.

“Katika kufikia malengo haya nguvu kazi yenye ujuzi rasmi na unaotambulika vya kutosha katika kumudu mahitaji ya soko la ajira inahitajika, ambapo kutokana na umuhimu huo serikali imeandaa programu ya kitaifa kwa miaka mitano ambayo itakuza ujuzi wa nguvu kazi hususan kwa vijana”, alisema.

Utekelezaji wa mpango huo alifafanua kuwa umeshaanza katika sekta mbalimbali kama vile ya nguo, ngozi, utalii, magari pamoja na kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi (RPL) wa mafunzo kwa vijana.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2014 Mhagama alisema kuwa idadi kubwa ya nguvu kazi iliyokuwa yenye sifa takribani asilimia 79.9 ina kiwango cha chini cha ujuzi na asilimia 16.6 ina kiwango cha kati na asilimia 3.6 ina kiwango cha juu cha ujuzi.

Kutokana na hilo uwiano huo alisema ni vigumu  kuweza kufikia azma ya uchumi wa viwanda na hatimaye nchi ya kipato cha kati kuwa na kiwango kinachotakiwa kutufikisha katika uchumi wa kati  cha uwiano wa asilimia 12 kwa ujuzi wa kiwango cha juu, asilimia 34 kiwango cha kati na kutozidi asilimia 54 kwa ujuzi wa kiwango cha chini.

Alisema kuwa uzinduzi wa awamu hii ya kwanza unarasimisha vijana 3,900 nchi kwa nzima kuanzia mwezi Julai hadi Oktoba   mwaka huu na baada ya hapo wataendelea na vijana wengine hadi wahakikishe kwamba vijana wote watakaokidhi vigezo husika wanatathiminiwa na kurasimishwa ujuzi.


Hali kadhalika Waziri huyo amevitaka vyuo vya VETA kuanzisha kozi nyingi zaidi ikiwemo ya utalii na kilimo ili wakulima wapate ujuzi utakaotosheleza na kuwezesha kuongeza uzalishaji mashambani na kuleta tija kupitia shughuli zao za kilimo.

No comments: