Monday, July 31, 2017

BUNDI ATUA KWA AFISA MISITU HALMASHAURI MJI WA MBINGA DC AAPA KUCHUKUA HATUA KALI ZA KISHERIA

Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Cosmas Nshenye wa pili kutoka kushoto akiwa ameshiriki katika kikao cha baraza hilo la Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga ambapo wa kwanza kutoka kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Robert Mageni na watatu kutoka upande huo wa kushoto ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ndunguru Kipwele. Upande wa kulia wa kwanza ni Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini, Sixtus Mapunda na wa pili yake ni diwani wa kata ya Luwaita Aureus Ndunguru ambaye alikuwa akikaimu kwa muda nafasi ya umakamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KUFUATIA kudaiwa kuwepo kwa ubadhirifu wa fedha za mapato yatokanayo na uvunaji wa msitu wa Mbambi uliopo katika kata ya Matarawe Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani humo Cosmas Nshenye naye ameapa akisema kuwa Ofisi yake itachukua hatua kali za kisheria ikiwemo kulifanyia uchunguzi jambo hilo na kulifikisha kwenye vyombo husika vya kisheria.

Nshenye alisema yeye binafsi hakubaliani na hali hiyo kwani dhahiri inaonesha kuwa kumekuwa na vitendo viovu ambavyo vinatia shaka juu ya mwenendo wa uvunaji wa msitu huo kwani ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu husika bila kufuata miongozo ya serikali umefanyika.

Mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo kilichofanyika mjini hapa, baada ya kuibuka hoja ya kumtuhumu Afisa misitu wa mji huo David Hyera kuwa anadaiwa kwa namna moja au nyingine kushiriki katika ubadhirifu wa mapato hayo.



“Mimi nilitarajia mtaalamu huyu wa misitu atatuambia ni kwa nini mbao nyingi zimetumika kwenye taasisi binafsi, hapa anatuletea taarifa ambayo haina ukweli juu ya uvunaji wa msitu huu badala yake anatumia mbinu za kusahisha mbele ya baraza hili, hii itakuwa ni taarifa ya uongo,

“Kwa sababu taarifa hii haijakaa vizuri nafikiri tungefikia maamuzi mimi nilazima suala hili nikalifanyie kazi kwanza zile shughuli za uvunaji mbao kule mlimani kuanzia sasa zisimame kwa maana ya kupisha uchunguzi ufanyike”, alisema Nshenye.

Katika hatua nyingine hata hivyo afisa huyo alisimamishwa kazi mbele ya baraza hilo ili aweze kupisha uchunguzi baada ya Madiwani hao kukubaliana kwamba iundwe Kamati maalumu itakayofanya kazi kwa kipindi cha mwezi mmoja kuchunguza tatizo hilo.

Nshenye aliwataka pia halmashauri wafanye uchunguzi wao peke yao na yeye ofisi yake itafanya uchunguzi wake binafsi na hatimaye endapo kutakuwa na ukweli juu ya jambo hilo wahusika watakaopatikana watafikishwa kwenye mkono wa sheria yaani Mahakamani ili kuweza kujibu tuhuma zinazowakabili.

“Niwaombe halmashauri mtengeneze timu ya kwenu ya uchunguzi na mimi nitengeneze timu ya kwangu, ili niweze kujua nawasilisha wapi na ninyi halmashauri mtajua mnawasilisha wapi”, alisema.

Vilevile kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini Sixtus Mapunda akichangia hoja katika kikao cha baraza hilo aliunga mkono mawazo yaliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Nshenye huku akieleza kuwa kamati hiyo itakayoundwa inapaswa kuitwa kamati maalumu ambayo itajumuisha wataalamu wa kutoka katika sekta mbalimbali ikiwemo mwanasheria wa halmashauri hiyo.

Pamoja na mambo mengine, ilielezwa kuwa makisio ya awali baada ya kufanyika upembuzi yakinifu na mtaalamu huyo wa misitu na kuwasilishwa katika kikao cha baraza la Madiwani kilichoketi Oktoba 12 mwaka jana, yalikuwa zipatikane zaidi ya shilingi milioni 325 ambazo ni baada ya uvunaji wa mbao katika msitu wa Mbambi kufanyika lakini walishangazwa kuelezwa kwamba zimepatikana shilingi milioni 196 ndipo mgogoro huo uliibuka ndani ya baraza hilo.

Naye Afisa misitu huyo, David Hyera alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya madai hayo alionekana kutoa taarifa ambazo zinapishana na maelezo ya awali yaliyonukuliwa kwenye makabrasha ya vikao vya madiwani hao, ambapo baadaye aliamrishwa akae chini na kuzuiwa asiongee chochote kutokana na takwimu zake alizokuwa akizitoa mbele ya baraza hilo kutoendana sawa na makubaliano ya vikao husika vilivyofanyika.

Mwenyekiti wa Kamati ya mipango miji na mazingira, Leonard Mshunju naye alithibitisha mbele ya baraza hilo huku akibainisha kuwa licha ya kutoa maazimio ambayo hata wafanyakazi waliofanya kazi ya uvunaji wa msitu ule wanapaswa kulipwa fedha zao, lakini hakuna kilichotekelezwa ambapo mpaka sasa bado wanadai zaidi ya shilingi milioni 20.

Mshunju alisema kuwa kamati yake ilizuiwa kwenda kukagua msitu huo kabla kazi ya uvunaji haijaanza kufanyika na kwamba licha ya kuomba wakaangalie nini kinachofanyika kule walikataliwa na hali hiyo alieleza kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu husika za baraza hilo.



No comments: