Monday, July 10, 2017

MWENYEKITI WA KIJIJI MATETELEKA MADABA LAWAMANI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda upande wa kulia, akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo pichani) eneo ambalo limekatwa miti kwa ajili ya shughuli za kilimo ambalo ni chanzo kikubwa cha maji katika kijiji cha Mwande kata ya Mateteleka ambapo mkazi mmoja, Regan Mlelwa amekata miti hiyo katika eneo hilo na kuathiri chanzo hicho cha maji, upande wa kushoto ni Mwenyekiti wa kijiji hicho Sosmo Dominicus.
Na Muhidin Amri,     
Madaba.

MWENYEKITI wa Serikali ya kijiji cha Mateteleka kata ya Wino Halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Remigius Njafula anatuhumiwa kugawa ardhi ya kijiji hicho kwa wageni, kinyume na taratibu husika jambo ambalo linasababisha kuzuka kwa mgogoro mkubwa kijijini hapo.

Wakitoa malalamiko yao mbele ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Shafi Mpenda, katika kikao kilichowajumuisha Wazee pamoja na uongozi wa kijiji wazee hao walifafanua kuwa vitendo hivyo vya dhuluma ya ardhi amekuwa akiwafanyia hasa wanawake na vijana.

Aidha wazee hao wamelalamikia kitendo cha Mwenyekiti huyo kutumia nguvu na kupokonya msitu wa kijiji ambao uliuzwa kwa kikundi cha Jitegemee kilichopo kijijini humo, miaka 15 iliyopita na kuanza kugawa maeneo ya msitu huo bila kushirikisha wamiliki husika.


Wakizungumza kwa niaba ya wazee wenzao mzee, Lucas Mayemba na Evolius Mbilinyi walisema kuwa Mwenyekiti huyo kwa kushirikiana na baadhi ya wajumbe wa serikali ya kijiji analalamikiwa pia kwa ubadhirifu wa shilingi milioni 9 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji na shilingi 600,000 zilizotolewa na mfuko wa Mbunge wa jimbo la Madaba na wahisani wengine kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya wanafunzi shuleni.

Walisema Njafula kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kijiji wamehamisha fedha na kwenda kuziweka kwenye akaunti ya mkandarasi kabla hajaanza kutekeleza mradi husika.

Kwa upande wake Mwenyekiti huyo alipoulizwa alikiri kuhamisha fedha hizo hata hivyo alieleza kuwa maamuzi hayo, yalifikiwa mbele ya mkutano mkuu wa kijiji ambao uliamua fedha zielekezwe huko ili kuepusha wajanja wachache kuzitafuna.


Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda mbali na kusikitishwa na tabia hiyo iliyofanywa na Mwenyekiti huyo ameahidi kulifikisha tatizo hilo kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukua mkondo wake.

No comments: