Tuesday, July 11, 2017

WAPOTEZA MAISHA BAADA YA PIKIPIKI WALIZOKUWA WAKIENDESHA KUGONGANA WAKIWA KATIKA MWENDO KASI

Na Muhidin Amri,       
Songea.        
    
WAENDESHA Pikipiki wawili wamefariki dunia baada ya Pikipiki zao walizokuwa wakiendesha kugongana wakiwa katika mwendo kasi katika kijiji cha Hanga kata ya Hanga wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Gemini Mushy alisema kwamba tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji hicho majira ya usiku.

“Vifo vya watu hawa vilitokea baada ya Pikipiki aina ya Yamaha yenye namba za usajili T 403 AGB iliyokuwa ikiendeshwa na Francis Mbawala (26) mkazi wa Mfaranyaki Hanga kugongana na Pikipiki nyingine ambayo haijafahamika namba zake za usajili”, alisema.

Kamanda huyo wa Polisi mkoani Ruvuma alifafanua kuwa Pikipiki nyingine ilikuwa ikiendeshwa na Sebastian Ngonyani (26) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Hanga kata ya Hanga wilayani Namtumbo, ambapo ilitoroshwa na watu wasiofahamika mara baada ya tukio hilo kutokea hata hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kuwatafuta watu waliotorosha Pikipiki hiyo.


Aidha alisema kuwa Pikipiki hizo zilikuwa na mwelekeo mmoja zikitokea kijiji cha Kitanda kuelekea Hanga na kwamba chanzo cha ajali hiyo ni ulevi baada ya waendesha Pikipiki hao kunywa pombe na kuendesha vyombo hivyo vya moto wakiwa katika mwendo kasi.

Kamanda Mushy ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto waache kutumia vileo wakati wanapoendesha vyombo hivyo, ili kuepusha kuweza kuleta madhara kama vile ulemavu au vifo.


Pamoja na mambo mengine amewataka madereva wa Pikipiki kuwasha taa muda wote wanapokuwa wanatumia vyombo hivyo wakiwa barabarani hasa nyakati za usiku, ili kuwezesha watumiaji wengine wa barabara kuweza kuona Pikipiki hizo zinapokuwa umbali mrefu na kuchukua tahadhari mapema kabla ya kuleta madhara.

No comments: