Monday, July 10, 2017

RC RUVUMA KUWACHUKULIA HATUA VIONGOZI WATAKAOZEMBEA KUSIMAMIA UKARABATI WA MAJENGO YA MAABARA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge upande wa kushoto akimsikiliza aliyekuwa Mkuu wa shule ya sekondari Ruanda, Stephano Ndomba wilayani Mbinga mkoani humo wakati alipokuwa juzi akitoa maelezo juu ya kuchelewa kwa ukarabati wa jengo la maabara la shule hiyo pamoja na jengo la kusomea wanafunzi wa kidato cha tano na sita.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka Wakurugenzi na Maafisa elimu Sekondari wa Halmashauri za wilaya mkoani humo, wahakikishe kwamba fedha zilizotolewa na serikali shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya shughuli ya ukarabati wa majengo ya maabara kwa shule hizo zinafanya kazi husika na sio vinginevyo.

Dokta Mahenge alitoa agizo hilo kwa kile alichoeleza kuwa anazotaarifa kwamba baadhi ya shule ambazo zimepelekewa fedha tokea mwezi Machi mwaka huu, kwa ajili ya kukarabati majengo ya kusomea wanafunzi wa kidato cha tano na sita pamoja na majengo ya maabara hakuna kazi zilizofanyika mpaka sasa.

Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa mkoa wakati alipofanya ziara yake ya kushitukiza katika wilaya ya Mbinga mkoani hapa, kwa lengo la kukagua ukarabati wa majengo ya shule ya sekondari Ruanda iliyopo katika kata ya Ruanda wilayani humo ambayo serikali imetoa shilingi milioni 259 kwa ajili ya kuweza kukamilisha kazi hiyo.


Aidha Dokta Mahenge alisikitishwa na kasi ya ukarabati wa majengo ya shule hiyo ambapo alieleza kuwa licha ya kupewa fedha hizo, hakuna kazi iliyofanyika na hilo lilitokana na viongozi husika kukaa muda mwingi ofisini bila kwenda kukagua maendeleo ya kazi hiyo.

“Ni lazima tunavyokuwa tumepanga mipango tunapaswa kukamilisha kwa wakati kama utekelezaji hakuna hapa hatuelewani, fedha hizi ziliingizwa kwenye akaunti ya shule hii muda mrefu lakini hakuna kazi iliyofanyika mnataka niwafanye nini?”, alihoji Dokta Mahenge.

Kwa upande wake alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya hali hiyo Afisa elimu wa shule za sekondari wilaya ya Mbinga, Joseph Kapere alisema kuwa ucheleweshaji huo wa ukarabati wa majengo hayo umetokana na miongozo husika ilichelewa kuwafikia ili waweze kufanya kazi hiyo.

Kapere aliongeza kuwa kutokana na kuchelewa kwa miongozo hiyo hawakuweza kufanya hata miamala ya fedha ambazo wangezitoa kwenye akaunti ya shule hiyo na kuweza kuanza kumlipa mkandarasi husika ili aweze kufanya kazi.  


Hata hivyo kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Mahenge alitoa mwezi mmoja kwa viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga wahakikishe kwamba ukarabati wa majengo kwa shule ya sekondari Ruanda unakamilika haraka iwezekanavyo na kwa viwango vinavyotakiwa na endapo usipofanyika hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

No comments: