Sunday, July 23, 2017

KOWELO ASHINDA NAFASI UMAKAMU MWENYEKITI KUONGOZA HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA


Zoezi la kuhesabu kura zilizopigwa na Madiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kumchagua Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo likifanyika jana katika ukumbi wa chama hicho uliopo mjini hapa chini ya usimamizi mkuu wa Katibu wa CCM wa wilaya hiyo, Zainabu Chinowa ambaye amesimama akiwa ameshika karatasi iliyokuwa tayari kura imepigwa.
Na Mwandishi wetu,   
Mbinga.

MADIWANI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamemchagua Joackimu Kowelo ambaye ni diwani wa kata ya Maguu kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo.

Uchaguzi huo ulifanyika jana majira ya asubuhi katika ukumbi wa CCM uliopo mjini hapa.

Katibu wa Chama hicho wilayani humo, Zainabu Chinowa ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, akitangaza matokeo hayo alimtaja Kowelo kuwa ndiye aliyeweza kushinda katika uchaguzi huo kwa kupata kura 26 dhidi ya mgombea mwenzake diwani wa kata ya Matiri, Benuward Komba aliyepata kura 7.


“Ndugu zangu uchaguzi umeenda vizuri tumeufanya kwa usalama na amani, wapiga kura walikuwa 34 kati ya hawa kura moja tu ndiyo iliyoharibika nadhani ni bahati mbaya ambayo inaonesha mpiga kura hakuwa na msimamo mzuri”, alisema Chinowa.


Hata hivyo pamoja na mambo mengine, chaguzi za kumchagua makamu Mwenyekiti wa kuongoza halmashauri ya wilaya zimekuwa zikifanyika kila baada ya mwaka mmoja na kwamba awali halmashauri ya wilaya ya Mbinga katika nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na diwani wa kata ya Matiri, Benuward Komba.

No comments: