Saturday, July 29, 2017

KUHAMISHWA WATUMISHI KADA YA AFYA KUNAKWAMISHA UTOAJI HUDUMA KWA WAGONJWA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KUFUATIA kuhamishwa kwa watumishi wa serikali kada ya afya waliokuwa wakitoa huduma kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati zilizokuwa chini ya mamlaka ya Jimbo Katoliki la Mbinga mkoani Ruvuma uongozi wa jimbo hilo unashindwa kuendelea kutoa huduma katika baadhi ya vituo vyake vya afya na hatimaye huenda vikafungwa wakati wowote kuanzia sasa na wananchi kukosa huduma husika.

Mwandishi wa habari hizi amebaini kuwa hata katika orodha ya watumishi hao ambao nakala yake tunayo, waliohamishwa wapo pia Watawa (Masista) kutoka mashirika mbalimbali katika jumuiya zao na kupelekwa kwenye vituo ambavyo havina Kanisa jambo ambalo imeelezwa kuwa ni kinyume na taratibu zao.

Vilevile kufuatia hali hiyo kumekuwa na mkanganyiko mkubwa kwa Wakuu wa mashirika ya jumuiya hizo na kuathiri kwa kiasi kikubwa huduma za afya zinazotolewa na Jimbo hilo kutokana na watumishi wengi kuhamishwa.


Mratibu wa afya Jimbo Katoliki la Mbinga, Padri Raphael Ndunguru alisema kuwa baadhi ya vituo hivi sasa wanapaswa kuvifunga mara moja kutokana na kukosa watumishi wenye sifa ya kuhudumia wagonjwa.

Alisema kuwa idara ya afya Jimbo Katoliki la Mbinga ambayo imeshirikiana vizuri na serikali kwa miaka mingi, leo inashangaa kuondolewa kwa watumishi hao wa serikali ambao walikuwa wameingia mikataba ya ubia baina yao na vituo hivyo binafsi.

“Kuondolewa kwa watumishi hawa Jimbo linaona kwamba ni ishara wazi kuwa huduma za afya tunazohudumia wananchi hazihitajiki tena, ikiwa na maana kwamba serikali ina uwezo mkubwa wa kuendelea kutoa huduma hizi hivyo sisi itatupasa kusitisha mara moja huduma tuzitoazo”, alisema Padri Ndunguru.

Alisisitiza kuwa katika kuendelea kujenga mahusiano mazuri ya kuhudumia wananchi, Jimbo linaiomba serikali iwarejeshe watumishi hao ili huduma za afya ziweze kuwa endelevu na wagonjwa wasiweze kupata usumbufu wa aina yoyote ile.

Pia Mwandishi wetu alipozungumza na Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko juu ya watumishi wa serikali kutokuendelea utiaji wa saini kwa mikataba mipya ya ubia na vituo vya kutolea huduma binafsi, alikiri kuwepo kwa jambo hilo na kukataa kutolea ufafanuzi licha ya ofisi yake ndiyo iliyohusika kutoa maagizo hayo ya kuhamisha watumishi hao.

Hata hivyo inathibitisha kuwa agizo hilo limetolewa na ofisi ya Katibu tawala huyo kupitia barua ya Aprili 18 mwaka huu ambayo nakala yake tunayo yenye kumbukumbu namba EC. 124/138/01/A/31 kwenda kwa Wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya mkoani humo kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo.


No comments: