Thursday, July 13, 2017

MANISPAA YA SONGEA YANUNUA MTAMBO WA KUZOLEA TAKA

Mtambo wa kisasa wa kuzolea taka ambao umenunuliwa na Manispaa ya Songea.
Na Mwandishi wetu,   
Songea

HATIMAYE Manispaa ya Songea iliyopo mkoani Ruvuma, imenunua mtambo wa kisasa wa kuzolea taka (kijiko) ambao kitaalamu unafahamika kwa jina la Back hoe Loader.

Afisa habari wa Manispaa ya Songea, Albano Midelo alisema kuwa mtambo huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 170 na kwamba umenunuliwa toka kampuni ya Hansom Tanzania Limited ya Jijini Dar es Salaam.

Midelo alieleza kuwa tayari mtambo huo umeanza kazi ya kukusanya taka katika viunga vya Songea mjini, hivyo kupunguza muda wa kuzoa taka kwa kutumia nguvu kazi.


Kwa mujibu wa Afisa habari huyo alisema kuwa Manispaa hiyo inazalisha taka kiasi cha tani 71.5 kwa siku ambapo uwezo wa Manispaa kuzoa taka kwa siku ulikuwa ni kati ya tani 35 hadi 40.

Kwa upande wake Afisa Usafi na mazingira wa Manispaa ya Songea, Philipo Beno alisema kuwa Manispaa ina jumla ya maghuba 33 ambapo baadhi ya maghuba yamebainika kuchangia uchafu wa mji.

Aliyataja maghuba hayo kuwa ni yaliyopo katika mtaa wa Mangolingoli, Sovi, Mchele na Mamboleo ambapo uongozi wa Manispaa unafikiria kuyaondoa maghuba hayo ili kuboresha usafi wa mji.

Beno aliongeza kuwa idara yake hivi sasa imeanza kuyaondoa maghuba yanayochafua hali ya mji, ambapo hadi sasa limeondolewa ghuba la stendi ya Bombambili na kwamba idara ina mpango pia wa kugeuza taka kuwa fursa kwa kutumia vikundi vya usafi wa mazingira.


Kwa ujumla Manispaa hiyo ina kata 21 na mitaa 95 huku ikiwa na jumla ya wakazi 218,942 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.

No comments: