Monday, July 24, 2017

MADIWANI HALMASHAURI MJI WA MBINGA WAMCHAGUA DIWANI KELVIN MAPUNDA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA HALMASHAURI HIYO

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kupitia Madiwani wake wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo ambao wanatokana na chama hicho, wamemchagua Kelvin Mapunda ambaye ni diwani wa kata ya Bethlehemu mjini hapa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji huo.

Kadhalika uchaguzi huo umefanyika leo majira ya asubuhi katika ukumbi wa CCM uliopo mjini hapa.

Aidha Katibu wa Chama hicho wilayani humo, Zainabu Chinowa ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, akitangaza matokeo hayo alimtaja Mapunda kuwa ndiye aliyeweza kushinda katika uchaguzi huo kwa kupata kura 13 dhidi ya mgombea mwenzake diwani wa kata ya Masumuni, Raphael Kambanga aliyepata kura 11.


Katika uchaguzi huo wapiga kura walikuwa 24 na kwamba chaguzi za kumchagua makamu Mwenyekiti wa kuongoza halmashauri ya mji huo, zimekuwa zikifanyika kila baada ya mwaka mmoja.


Pamoja na mambo mengine hapo awali halmashauri ya mji wa Mbinga katika nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na diwani wa kata ya Kikolo, Tasilo Ndunguru ambaye kwa awamu hii hakuchukua fomu ya kugombea tena nafasi hiyo.

No comments: