Tuesday, July 11, 2017

MGODI WA NGAKA MBINGA WAKABILIWA NA CHANGAMOTO KUBWA KATIKA SOKO LA KUUZA MAKAA YA MAWE HAPA NCHINI

Aliyesimama ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge akizungumza juzi wakati alipokuwa akitaka ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali ya maendeleo ya soko la usafirishaji wa makaa ya mawe ambayo yanasafirishwa kwenda kwa watumiaji waliopo hapa nchini, ambayo yanachimbwa na kuzalishwa na Kampuni ya Tancoal Energy katika Mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilaya ya Mbinga mkoani humo.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa uzalishaji wa makaa ya mawe yanayochimbwa katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, unakabiliwa na changamoto kubwa ya soko la kuuzia makaa hayo kutokana na viwanda vinavyotumia nishati hiyo hapa nchini kupunguza kasi ya ununuaji wa mkaa huo.

Aidha imefafanuliwa kuwa viwanda vya saruji ambavyo kwa kiasi kikubwa vilikuwa vikitumia mkaa huo, hivi sasa vimekuwa vikinunua kiasi kidogo cha mkaa jambo ambalo limekuwa likisababisha kuyumba kwa soko la ndani la bidhaa hiyo.

Hayo yalisemwa na Kaimu Meneja wa Kampuni ya Tancoal Energy, Edward Mwanga baada ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge kutembelea mgodi huo juzi kwa lengo la kutaka kujiridhisha juu ya hali ya uzalishaji wa mkaa huo.


Mwanga alisema kuwa uzalishaji hivi sasa umekuwa mkubwa ambapo kwa siku wamekuwa wakichimba tani 2,000 hadi 2,500 lakini changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni wateja waliopo hapa nchini huyatumia makaa hayo kwa kiasi kidogo tofauti na uzalishaji wanaoufanya.

“Hivi sasa uzalishaji tunaoufanya kinachotuyumbisha hapa ni soko la kuyauza kwa ujumla uzalishaji wa mkaa umekuwa mkubwa hakuna tatizo, kwa takwimu nilizonazo hapa ndani ya mwezi tumekuwa tukizalisha tani 60,000 na kuendelea”, alisema Mwanga.

Alisema kuwa hapo awali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kutembelea mgodi huo aliwataka kuboresha mitambo na kuongeza kasi ya uzalishaji wa mkaa, hivyo wameweza kutekeleza agizo la Waziri huyo lakini kinachowayumbisha ni wapi kwa kwenda kuyauza makaa hayo kutokana na soko la ndani kutokuwa na uwezo wa kuyanunua.

Hapo awali alieleza kuwa walikuwa wakizalisha tani 80 hadi 100,000 kwa mwezi lakini hivi sasa tatizo hilo halipo tena kutokana na kuongeza mitambo hiyo ya uzalishaji.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo, Dokta Mahenge mara baada ya kushuhudia uzalishaji unaofanywa kwenye mgodi wa Ngaka, aliyaomba makampuni na wawekezaji wenye viwanda mbalimbali hapa Tanzania kwenda kununua mkaa huo ili waweze kuendeshea mitambo ya viwanda vyao kwani uzalishaji wa mkaa umekuwa mkubwa tofauti na hapo awali.


“Niwaombe wawekezaji wetu wajitokeze kwa wingi kuja kununua makaa haya ili tuweze kukuza soko letu la ndani, hivi sasa hakuna matatizo tena ya uzalishaji wa mkaa katika mgodi huu”, alisema Dokta Mahenge.

No comments: