Tuesday, July 11, 2017

RC RUVUMA AWAJIA JUU WATENDAJI WA SERIKALI AWATAKA WABADILIKE WAENDANE NA WAKATI


Msafara wa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge ukiwa katika kazi ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni la shule ya sekondari ya wasichana Mbinga iliyopo katika kata ya Kigonsera wilaya ya Mbinga mkoani humo. (Picha zote na Gwiji la Matukio Ruvuma)
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

VIONGOZI ambao wamepewa dhamana na serikali ya kuongoza Halmashauri za wilaya mkoani Ruvuma, wameonywa kuacha mara moja tabia ya kukaa muda mwingi Ofisini badala yake watembelee na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi vijijini ili iweze kujengwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Onyo hilo limetolewa juzi na Mkuu wa mkoa huo, Dokta Binilith Mahenge wakati alipokuwa wilayani Mbinga katika ziara yake ya kukagua baadhi ya miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya shule za sekondari wilayani humo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa umefika wakati sasa kwa kila kiongozi aliyekuwa katika nafasi yake mkoani humo anapaswa kutekeleza ipasavyo majukumu aliyopewa na serikali, ili kuweza kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano hususan katika kukuza sekta ya elimu kwa faida ya kizazi cha sasa na kile kijacho.


“Nimetembelea baadhi ya shule zetu za sekondari hapa Mbinga nahitaji kuona kasi ya kusimamia ukarabati na ujenzi wa majengo ya shule hizi uwe mzuri, natoa mwezi mmoja kuanzia sasa nitakapofika siku nyingine kukagua tena nikute kazi zilizopangwa kufanyika ziwe zimetekelezwa ipasavyo, vinginevyo viongozi mliopewa dhamana mjiandae kuwajibishwa na hili ni agizo la mkoa mzima”, alisisitiza Dokta Mahenge.

Vilevile kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye akichangia hoja wakati wa kuhitimisha ziara hiyo alimweleza Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Mahenge kwamba yeye na viongozi wenzake wilayani humo watahakikisha wanazingatia maagizo hayo ikiwemo kusimamia vizuri miradi yote ya wananchi iliyotengewa fedha na serikali ili iweze kutekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.

“Maswali yote yaliyoulizwa leo hapa yalitakiwa yajibiwe na watu wa Ofisi ya mipango niwaombe badala ya kuwataka, Ofisi hii ijipange upya kufanya ufuatiliaji na itoe taarifa kwa sababu inaonekana kuna mambo yanafanyika kwa wananchi kule vijijini lakini hatuyafahamu”, alisema Nshenye.

Kwa ujumla mkoa wa Ruvuma hivi sasa una wilaya sita ambazo ni wilaya ya Songea, Mbinga, Tunduru, Namtumbo, Nyasa na Madaba zikiwemo pamoja na Manispaa ya Songea na halmashauri ya mji wa Mbinga. 

No comments: