Sunday, July 30, 2017

TANZANIA NA MSUMBIJI WATAKIWA KUPAMBANA NA TATIZO LA UMASKINI

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dokta Binilith Mahenge upande wa kushoto akiwa na Gavana wa Jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbuji Celmira Da Silva upande wa kulia, juzi wakitiliana saini makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa pamoja wa ujirani mwema na uhusiano kati ya mikoa ya Mtwara na Ruvuma kwa upande wa Tanzania pamoja na majimbo ya Cabo Delgado ya nchini Msumbiji.
Na Muhidin Amri,         
Songea.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge amewataka wananchi na viongozi wa Tanzania na Msumbuji kuhakikisha kwamba wanapambana na tatizo la umaskini ambao umekithiri katika nchi zao, ili kuweza kuendelea kuwa na hali ya amani na utulivu katika nchi hizo.

Dokta Mahenge alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akifunga mkutano wa ujirani mwema ambao ulishirikisha mikoa ya Ruvuma na Mtwara upande wa Tanzania na Jimbo la Niassa na Cabo Delgado nchini Msumbiji ambao ulifanyika juzi kwenye ukumbi wa Hunt Club uliopo mjini Songea mkoani Ruvuma.

“Kinachohitajika hivi sasa ni viongozi kushirikiana na wananchi kwa pande zote mbili na kuhakikisha mnasimama imara ili tuweze kufanya kazi kwa bidii na kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani, hatua ambayo itasaidia vijana kujiepusha na vitendo vya uharibifu na ujangili”, alisema.


Alisema kuwa endapo hapatakuwa na mshikamano na utulivu huu uliopo sasa wahalifu watakuwa na nafasi kubwa ya kuvuka mipaka na kujificha nchi jirani, kwa lengo la kuvuruga amani iliyopo na hatimaye kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Pia alibainisha kuwa harakati za wananchi kujiletea maendeleo hazitafanikiwa endapo masuala ya usalama wa mipaka ya nchi hizo yatavurugwa, hivyo pande zote mbili zitaendelea kuwa na umaskini.

Dokta Mahenge alisema kuwa hakuna sababu ya watu wa Msumbuji kuagiza chakula kutoka nchi za Ulaya, kwa sababu Tanzania ndani ya mkoa wake wa Ruvuma kuna chakula cha kutosha kinachoweza kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Naye Gavana wa Jimbo la  Cabo Delgado nchini Msumbuji, Celmira Frederico Pena da Silva alisema kuwa hivi sasa kazi kubwa iliyopo wanatakiwa kuendelea kudumisha amani kwa pande zote mbili na kuwawezesha wananchi kukua kiuchumi.


Vilevile kwa upande wake Gavana wa Jimbo la Niassa Alindo Chilundo aliongeza kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016/2017 wananchi wa  jimbo hilo walifanikiwa kuzalisha zaidi ya tani milioni 5 za mahindi na kuwataka wafanyabiashara kutoka Tanzania kwenda Msumbiji kununua  zao hilo ikiwa ni njia mojawapo ya kudumisha umoja na uhusiano uliopo miongoni mwao.

No comments: