Monday, July 10, 2017

MKURUGENZI MTENDAJI MADABA AKIFUNGA KITUO CHA UTAFITI WA SAYANSI NA TIBA ASILI

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda upande wa kulia, akimbana mmiliki wa kituo cha kutibu magonjwa mbalimbali kwa kutumia dawa za mimea, chakula na matunda cha The King Solomon of Sanitarium Clinic upande wa kushoto ambaye ni mfanyakazi wa kituo hicho, Ezakiel Mwakatumbula (26) kabla ya kufunga kituo hicho baada ya kufanya shughuli zake bila kufuata sheria na taratibu husika.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda akifunga kituo cha The King Solomon Sanitarium Clinic ambacho kinatoa huduma za matibabu kwa kutumia dawa za mimea, matunda na matunda kilichokuwa kikifanya shughuli zake bila kuwa na leseni inayoruhusu kufanya kazi hiyo.
Na Muhidin Amri,        
Madaba.

KITUO cha utafiti wa Sayansi tiba asili kinachofahamika kwa jina maarufu la The King Solomon of Sanitarium, ambacho kinajishughulisha na upimaji wa afya za binadamu na kutibu magonjwa mbalimbali katika wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma, kimefungwa kisiendelee kutoa huduma hizo hadi pale Wataalamu wa afya watakapojiridhisha na uhalali wa uwepo wake wilayani humo.

Aidha hatua ya kukifunga huko imetekelezwa juzi na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Shafi Mpenda baada ya kubaini mapungufu husika ikiwemo kutokuwepo kwa vibali halali vinavyoruhusu kituo hicho kufanya kazi hizo.

Mbali na hayo Mpenda alisema kuwa atawachukulia pia hatua kali baadhi ya wataalamu wake wa idara ya afya, ambao wanadaiwa kushiriki kutoa vibali feki vilivyoruhusu kituo hicho kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa mmiliki wa kituo cha The King Solomon of Sanitarium, Seleman Nzaganya amekuwa akifanya shughuli zake kinyume na taratibu ambapo hata leseni kutoka Baraza la tiba asili imekwisha muda wake tangu ilipofika mwezi Januari mwaka huu na kwamba, amekuwa akiendelea kufanya shughuli za upimaji wa afya za binadamu bila kuwa na leseni mpya jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.


“Nimelazimika kukifunga kituo hiki ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi kwani inaonesha wamekuwa wakifanya kazi zao kwa mtindo wa kutapeli wananchi kwa sababu hata mtu tuliyemkuta akihudumia wagonjwa, hana taaluma yoyote ile inayomwezesha kutoa huduma jambo ambalo ni hatari kwa afya ya binadamu”, alisema Mpenda.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa hii ni mara ya pili kufunga kituo kama hicho na kwamba ni kampeni endelevu kwa  wale wote wanaowatapeli wananchi wa wilaya ya Madaba, huku akitoa onyo kali kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo kuacha mara moja na watafute maeneo mengine ya kufanya shughuli zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotaja majina yao ambao ni wakazi wa wilaya hiyo walipongeza hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ambayo inalenga kuokoa maisha ya watu wake.

Walisema kituo hicho kilikuwa sehemu ya tatizo kwani hata wananchi waliokuwa wakienda hapo kwa ajili ya kupata ushauri na matibabu, wamekuwa wakiamini kwamba watapata suluhu ya matatizo yao kumbe wamekuwa wakizidisha ukubwa wa matizo waliyonayo.

Kwa upande wake akizungumza kwa niaba ya mmiliki wa kituo hicho, mtu mmoja aliyekutwa akitoa huduma katika kituo hicho Ezakiel Mwakatumbula alipohojiwa na mwandishi wetu alisema kuwa wamekuwa wakitoa huduma za matibabu kwa magonjwa mbalimbali hasa magonjwa sugu kwa kutumia dawa za mimea, chakula na matunda.


Hata hivyo alikanusha kufanya shughuli zao kitapeli huku akisisitiza kwamba, huduma wanazotoa zimekuwa zikiwasaidia wananchi wengi katika kuokoa maisha yao pale wanapougua.

No comments: