Wednesday, July 26, 2017

WANANCHI MKOA WA RUVUMA WATAKIWA KUWA NA MAZOEA YA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Binilith Mahenge.
Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

DOKTA Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa mkoa wa Ruvuma amewahimiza Wananchi wa mkoa huo, kuwa na tabia yenye mazoea ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani humo badala ya kuwaacha wageni peke yao wakitumia fursa hiyo.

Mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, huku akisisitiza kwamba ndani ya mkoa huo kumekuwa na vivutio vingi ambavyo vikitumika vyema vitasaidia kukuza pato la mkoa na maendeleo ya wananchi wake.

“Vivutio hivi vikitumika ipasavyo vitaufanya hata mkoa wetu kupata wageni ambao watachangia kukua kwa uchumi na pato la serikali na pia naviomba vyombo vya habari hakikisheni mnatangaza fursa hizi kama vile mbuga ya Selou, Ziwa Nyasa, Jiwe la Mbuji lililopo Mbinga ambalo linatajwa kuwa ndiyo refu kuliko yote hapa nchini na vivutio vingine tulivyonavyo”, alisisitiza Dokta Mahenge.



Dokta Mahenge aliongeza kuwa juhudi zinaendelea kwa serikali ya mkoa wa Ruvuma kuhakikisha kwamba vivutio vilivyopo vinakuwa katika mazingira rafiki ya kufikiwa na watu kutoka maeneo mbalimbali, tofauti na sasa ambapo baadhi ya maeneo hayo hayafikiki kwa urahisi kutokana na miundombinu yake kama vile barabara kuwa mibovu.

No comments: