Thursday, September 3, 2015

ACHOMWA KISU UBAVUNI KUTOKANA NA WIVU WA KIMAPENZI

Hiki ni kisu ambacho kinadaiwa kutumika katika tukio hilo.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

ATHUMAN Namamba (22) mkazi wa kijiji cha Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amenusurika kupoteza maisha baada kuchomwa kisu katika ubavu wake wa kushoto katika tukio linalodaiwa chanzo chake, ni wivu wa kimapenzi.

Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya wilaya hiyo na hali yake ni mbaya, ambapo kisu hicho alichomwa na Halid Sinda mkazi wa kijiji hicho Agosti 16 mwaka huu, majira ya usiku baada ya kutokea mabishano kati yao ambapo mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu majeruhi huyo kwamba ana mahusiano ya kimapenzi na mchumba wake, Mwajuma Ndeka.

Taarifa zinaeleza kuwa mtuhumiwa, Sinda aliendeleza jazba na akafikia hatua ya kuchomoa kisu na kumchoma nacho, Athuman hali ambayo ilisababisha kutoka damu nyingi na kumsababishia maumivu makali.


Mtuhumiwa ametokomea kusikojulikana na kwamba Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha juu ya tukio hilo na anaendelea kutafutwa hivyo atakapopatikana hatua za kisheria, zitachukuliwa dhidi yake.

Kadhalika Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta Mmari Zabron alisema amempokea majeruhi huyo na kuongeza kuwa maafisa tabibu wanaendelea na jitihada ya kuokoa maisha ya majeruhi huyo.


Alibainisha kuwa ameumizwa vibaya katika ubavu huo wa kushoto na kukatwa baadhi ya viungo vilivyomo ndani ya mwili, kutokana na kuchomwa kisu hicho.

No comments: