Sunday, September 13, 2015

TUNDURU WAISHUKIA UKAWA WAPONDA KUPOKELEWA KWA LOWASSA

Wananchi wakiwa katika mikutano mbalimbali ya kisiasa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Na Muhidin Amri,
Tunduru.

WANACHAMA 153 kutoka Chama cha wananchi CUF na CHADEMA katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wamevihama vyama hivyo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa wamechoshwa na siasa zisizokuwa na malengo kwa Watanzania, pamoja na udikteta unaofanywa na viongozi wa vyama hivyo kufanya maamuzi mbalimbali bila kushirikisha wanachama wao.

Miongoni mwa wanachama hao, 120 ni wa kutoka CUF na 33 CHADEMA walitangaza juzi kuhama katika vyama hivyo, mbele ya katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa wilaya hiyo, Mohamed Lawa tukio ambalo liliambatana na kurudisha kadi za vyama hivyo.

Walisema kuwa kwa muda mrefu sasa vyama hivyo vimekosa demokrasia ya kweli, ambapo viongozi wake ni watu ambao wamekuwa wakifanya maamuzi ambayo yamekuwa kinyume na matarajio ya watanzania walio wengi, wanaohitaji maendeleo.

Waliongeza kuwa hata kupokewa kwa Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na hatimaye kuwa mgombea urais wa Ukawa, ni udhaifu alionao Freeman Mbowe, James Mbatia na Maalim Seif Sharif kwani hapakuwa na sababu ya wao kumpokea Lowassa kwani mgombea wa kiti hicho hajawahi kukanusha wala kuwaeleza wananchi, ukweli juu ya tuhuma za ufisadi zilizomkabili akiwa ndani ya CCM.


Aidan Mbawala na Khalfan Wilis kutoka CHADEMA walieleza kuwa viongozi wao wa Ukawa hawajatenda haki kwa wanachama wao, ambapo walitakiwa kwanza kupata maoni kutoka kwao juu ya uhalali wa Lowassa kama anafaa kujiunga na umoja huo, huku wakidai kuwa hayo ni matokeo ya ubinafsi na tamaa ya fedha ambazo wanaimani wamepewa au kuahidiwa na mgombea huyo.

Walidai kuwa Mbowe na Mbatia ni watu ambao wanapenda sana fedha, hivyo ujio wa Lowassa sio jambo geni kwao kwani ikumbukwe kwamba alipoenguliwa na CCM katika kinyang’anyiro cha kugombea nafasi hiyo, alikwisha tangaza kuwa hawezi kukihama chama hicho.

Nao wanachama kutoka CUF, Yasin Jafar na Ahamad Issa walisema wamechukua jukumu la kurudisha kadi na kujiunga na chama tawala baada ya kuchukizwa na uamuzi wa viongozi hao, kumshawishi na kumpokea Lowassa kwenda huko jambo ambalo hata viongozi wenzao ngazi ya juu wamekuwa wakilipinga.

Mbali na hilo wanachama hao wamempongeza Dokta Wilbrod Slaa na Profesa Haruna Lipumba kwa maamuzi mazuri waliyochukua, kuhama kwenye vyama hivyo vinavyounda Ukawa kwani viongozi wanaounda umoja huo hakuna hata mmoja mwenye sifa ya kuwaongoza watanzania, kutokana na tabia ya ubinafsi na tamaa ya fedha waliyonayo.

Pia Hamad Issa amewatahadharisha wanachama wenzao, wa kutoka vyama vya upinzani kuwa macho na viongozi wao kwa kile walichodai kuwa wanaweza kuwapotezea muda wao, hasa baada ya kuonekana hawana nia njema kwa wananchi bali wapo kwa maslahi yao binafsi.

Alipokuwa akiwapokea wanachama hao, Katibu wa CCM wilaya ya Tunduru Mohamed Lawa licha ya kuwapongeza amewataka kujenga ushirikiano na wanachama wenzao wa chama hicho tawala, kwa kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.


Lawa alisema chama hicho, kimejipanga kikamilifu kuhakikisha ushindi unapatikana kwenye uchaguzi huo kwa nafasi ya Ubunge, Diwani na Rais huku akiwataka wagombea kujiepusha na lugha za matusi wanapokuwa jukwaani badala yake wajenge hoja zitakazowashawishi wananchi, kuwapigia kura.

No comments: