Friday, September 4, 2015

WATAKIWA KUFANYA KAMPENI ZA KIUSTAARABU

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

VIONGOZI wa vyama mbalimbali vya siasa hapa Tanzania, wameendelea kushauriwa kufanya mikutano yao ya kampeni za siasa kiustaarabu, katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, bila kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo hapa nchini.

Mkurugenzi wa shirika la maendeleo, mikoa na matawi ya Tanzania Red cross Society, Julius Kejo alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wadau wa shirika hilo kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo, jinsi ya kukabiliana na majanga wakati wa kampeni hizo.
Aidha aliwakumbusha viongozi wa dini, kuongeza juhudi na kutoa mahubiri yanayolenga kusisitiza amani na utulivu katika nchi yetu, ili isiweze kujitokeza machafuko yanayoweza kuliangamiza taifa hili.

Kejo alisema endapo kampeni hizo zitafanyika bila kuathiri ubinadamu au utu wa mtu, upo uwezekano wa kutotokea matendo ambayo yanaweza kusababisha madhara katika jamii.


Alifafanua kwamba shirika lake litaendelea kuimba wimbo wa amani na utulivu kwa watanzania, na kuongeza kuwa mafunzo hayo yamekwisha tolewa kwa wadau wengine wa maeneo ya Mtwara, Dar es Salaam, Iringa na Songea kwa lengo la kuwaweka tayari ili waweze kukabiliana na matukio ya uchaguzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilayani Tunduru, Nyenje Undi aliwatupia viongozi wa chama tawala CCM, akidai kuwa ndiyo wamekuwa wakivitumia vibaya vyombo vya dola likiwemo jeshi la Polisi ambalo badala ya kutenda haki limekuwa likivikandamiza vyama vya upinzani, kwa kutumia mabavu na vipigo kwa raia wasiokuwa na makosa kitendo ambacho kinasababisha uvunjifu wa amani.

Akijibu juu ya hilo, mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, SP. Nico Mwakasanga alisema kuna kila sababu jamii kutii sheria bila shuruti pale amri inapotolewa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kulisaidia shirika la Red cross kutofanya shughuli za uokoaji wa majanga ambayo yamekuwa yakisababishwa na vipigo vya Polisi.

Mwakasanga alibainisha kuwa tayari Jeshi hilo limekwisha fanya kazi ya kutoa elimu kwa askari wake, juu ya matumizi ya nguvu kwa wananchi hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu huku akiongeza kuwa, askari atakayekikuka maelekezo husika atachukuliwa hatua za kisheria.

Upande wa viongozi wa madhehebu ya dini ambao waliwakilishwa na mchungaji Myiya Kashimito wa kanisa la Biblia Tunduru na Shekh Abdalah Mdidu, waliahidi kuongeza juhudi katika kutimiza wajibu wao na kwamba wakati wote wataendelea kuhubiri amani na utulivu.


Awali akifungua mafunzo hayo Mwenyekiti wa shirika hilo wilayani humo, Rashid Mchileka aliwataka Wadau wake kuwa wajumbe wazuri katika kusambaza elimu watakayoipata, ili kuweza kuepusha jamii isiweze kujiingiza kwenye makundi mabaya yatakayoweza kusababisha vurugu.

No comments: