Wednesday, September 23, 2015

AKAMATWA KWA KURUSHIA MAWE MSAFARA WA KAMPENI WA CCM

Na Kassian Nyandindi,
Songea.

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma limesema, limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya watano ambao walihusika katika tukio la kurushia mawe msafara wa kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mtua, kata ya Mpepai wilayani Mbinga mkoani humo na kuharibu magari mawili.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Revocatus Malimi alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu na kuongeza kuwa katika tukio hilo wengine watano, wametokomea kusikojulikana ambapo wanaendelea kuwasaka ili waweze kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria, kujibu tuhuma inayowakabili.

Malimi alisema usiku wa kuamkia Septemba 22 mwaka huu, askari wake walifanya msako mkali katika kata hiyo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja kati ya hao, aliyemtaja kwa jina la Christopher Mapunda (32) ambaye ni mkazi wa kijiji hicho.


Magari mawili yameharibiwa vibaya, baada ya watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuvamia msafara huo na kurusha mawe huku watu waliokuwemo ndani ya magari hayo nao wakinusurika kujeruhiwa.

Alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo aliyekamatwa, ndiye aliyekuwa kiongozi wa kuwahamasisha watuhumiwa wenzake warushie mawe msafara huo wa kampeni za CCM, katika kata hiyo ya Mpepai na kwamba wakati wowote kuanzia sasa atafikishwa Mahakamani.


Hata hivyo, magari ambayo yaliharibiwa ni pamoja na gari la Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga lenye namba za usajili T 545 BEW aina ya Landcruiser Hardtop limevunjwa kioo cha ubavuni upande wa kushoto na lingine aina ya Landrover Discover, lenye namba T 797 AEN nalo limevunjwa vunjwa vioo kwa mawe ambayo yalikuwa yakirushwa.

No comments: