Tuesday, September 22, 2015

UVCCM TUNDURU YAWAONDOLEA HOFU WANANCHI SIKU YA KUPIGA KURA

Katibu mkuu Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM), Sixtus Mapunda.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewataka wanachama wake na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi na kwenda kupiga kura bila uoga wala hofu ya aina yoyote, kwa lengo la kumchagua kiongozi wanayemtaka Oktoba 25 mwaka huu.

Katibu wa UVCCM wilayani humo, Juma Khatibu alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliohudhuria kwenye mkutano wa kampeni wa kuwanadi wagombea udiwani, katika kata za Masonya, Majengo na Mlingoti Mashariki mjini hapa.

Alisema kuwa umoja huo umechukua hatua hiyo, kufuatia kuwepo kwa taarifa za vitisho ambavyo husambazwa kwa njia ya vipeperushi wilayani humo, zenye nia ya kuwatia hofu wananchi wasipige kura.


Khatibu alieleza kuwa watu walio katika makundi maalumu kama vile wazee na walemavu, wamekuwa wakitishwa kwamba siku hiyo ya uchaguzi kutakuwa na makundi ya vijana ambayo yameandaliwa kuleta fujo, zitakazowazuia wasipige kura za wagombea waliosimamishwa na CCM.


Alibainisha kuwa katika kuwahakikishia ulinzi na usalama siku hiyo, umoja huo umekwisha andaa makamanda 11,876 ambao watasambazwa kama wasimamizi na walinzi wa kura za chama hicho tawala, katika vituo vyote vya kupigia kura.

No comments: