Friday, September 11, 2015

NAMTUMBO WAITAKA SERIKALI KUYADHIBITI MAKAMPUNI YANAYONUNUA TUMBAKU

Mkulima akiwa katika shamba la tumbaku akiboresha zao hilo.
Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.

WAKULIMA wanaozalisha zao la tumbaku wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, wameitaka serikali kuhakikisha inadhibiti ipasavyo tabia ya makampuni binafsi yanayonunua zao hilo wilayani humo kwa njia za ujanja ujanja, yanachukuliwa hatua za kisheria kwani utekelezaji huo usipofanyika mapema huchangia kwa kiasi kikubwa, kuwaibia wakulima na kuwaacha wakibaki maskini.

Aidha walieleza kuwa kumekuwa na mtindo unaotumika wakati wa kununua zao hilo kwa kutumia fedha za kigeni, jambo ambalo wakulima wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya kiwango halisi cha thamani ya fedha anayotakiwa kulipwa mkulima husika.

Baadhi yao walisema wanakabiliwa na tatizo hilo, kutokana na wengi wao wanaolima tumbaku kutofahamu mabadiliko ya fedha hizo pale wanapolipwa na makampuni hayo, wakati wa msimu wa mauzo ya zao hilo.


Mmoja wa wakulima wa kijiji cha Matepwende wilayani Namtumbo, Abdalah Ngonyani alisema makampuni hayo yamekuwa yakitumia fedha hizo maarufu kwa jina la dola, kuwalipa wakulima hali hiyo wanaiona ni sawa na kuwaibia kutokana na wengi wao huishi mashambani na huchukua muda mrefu kwenda mjini kufuata huduma za kibenki, ili waweze kubadilisha fedha hizo kuwa shilingi ya kitanzania kwa ajili ya kuweza kununua mahitaji yao muhimu.

Walisema wao wanachotambua fedha hizo zinamtindo wa kubadilika kila mara kulingana na mfumo wa soko au kuporomoka kwa uchumi wa dunia, hivyo wameona sio jambo jema kwa makampuni hayo kuendelea kununua tumbaku kwa fedha hizo za kigeni, ambazo baadaye mkulima hupata usumbufu pale anapohitaji kubadilisha kuwa shilingi.

Pamoja na mambo mengine katika msimu huu wa 2015/2016, wameitaka serikali kusimamia kidete suala hilo, ili mkulima aweze kuondokana na adha hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Ali Mpenye alisema tayari ofisi yake imekwisha waandikia barua watendaji wa vijiji na kata, kuwajulisha kwamba hakuna mfanyabiashara wa mazao anayeruhusiwa kununua mazao kutoka kwa mkulima kwa kutumia fedha za kigeni.

Mkurugenzi huyo alisema iwapo mtu au mfanyabiashara yeyote ambaye atabainika kufanya hivyo, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo wanapaswa kutumia kibali husika ambacho hutolewa na halmashauri hiyo na matumizi sahihi ya mizani ambayo hutumika wakati mazao hayo yanaponunuliwa kutoka kwa mkulima.
 

No comments: