Monday, September 7, 2015

WAKULIMA WANAOZALISHA MUHOGO WAASWA

Vichanja bora vya kukaushia mihogo.
Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa ubunifu na maeneo ya kufanyia biashara kwa wasindikaji wadogo, bidhaa zitokanazo na zao la muhogo wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma kunasababisha kuongezeka kwa watu maskini kutokana na wakulima husika katika maeneo mengi ya wilaya hiyo, kukosa mbinu na utaalamu wa kilimo cha zao hilo na kujikuta wakipoteza nguvu na muda mwingi wa kufanya kazi hiyo.

Aidha uzalishaji usiozingatia viwango vyenye ubora nayo ni sababu nyingine, ambayo mkulima wa zao hilo anakosa mafanikio, licha ya jitihada na nguvu kubwa anayoitumia wakati anapozalisha zao hilo.

Mbali na hilo usindikaji umekuwa ukifanywa kwa kutumia vifaa duni, tatizo ambalo limekuwa likichangia bidhaa zinazozalishwa kutokana na muhogo kukosa soko la uhakika, na wakulima kuendelea kuwa masikini ikilinganishwa na wakulima wanaozalisha mazao mengine.


Hayo yalisemwa na Mratibu wa mradi wa Muunganisho Ujasiriamali Vijijini (MUVI) mkoani Ruvuma, Ralph Kananga alipokuwa akitoa mafunzo ya uboreshaji wa zao la muhogo na bidhaa zake kwa wajasiriamali wadogo, kutoka vikundi vitano vilivyomo wilayani humo.

Kananga alibainisha kuwa licha ya kazi kubwa wanayoifanya wakulima hao, bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo zana duni, maeneo ya kufanyia biashara na kuendelea kusindika kwa kutumia njia za kizamani.

Baadhi ya changamoto zinachangiwa na wakulima wenyewe hujikuta bado wanaendelea kubaki kuwa maskini wa kipato, licha ya ukweli kwamba zao la muhogo ni kati ya mazao yenye soko kubwa hapa nchini, na ulimwengu kwa ujumla.

Aidha wakulima wameshauriwa kuongeza jitihada katika uzalishaji wa mazao bora ya muhogo na kuahidi kuwa MUVI, itaendelea kuwaunga mkono katika mpango wao wa kupunguza umasikini kupitia kilimo cha muhogo kwa kutoa mafunzo na mbinu mbalimbali, ambazo zitasaidia kuinua hali zao za maisha.

Mratibu huyo alieleza kuwa mradi utaendelea kuifanya wilaya ya Namtumbo, kutambulika kimataifa kutokana na zao hilo ambalo wadau mbalimbali wa ndani na nje, kwenda katika wilaya hiyo kujionea na kujifunza juu ya kilimo cha muhogo.

Kutokana umuhimu huo wakulima waliojiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali kutokata tamaa na hali hiyo, badala yake waongeze juhudi kutokana na MUVI itaendelea kuwa pamoja nao kwa kutoa ushauri, kuwatafutia masoko na kuwajengea uwezo ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki yatakayowafanya waweze kunufaika nayo juu ya kilimo cha zao hilo.


Hivi sasa MUVI inafanya kazi katika mikoa mitatu ya Pwani, Ruvuma na Mwanza ambapo katika mkoa wa Ruvuma inafanya kazi zake wilaya ya Songea, Namtumbo na Mbinga jambo ambalo limeifanya kufanikiwa katika kuongeza ubora wa zao hilo.

No comments: