Sunday, September 27, 2015

BEROYA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA UDANGANYIFU WA MITIHANI

Ofisa elimu Sekondari Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Leo Mapunda kushoto, akimsikiliza mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Beroya, Mary Komba namna ya kupima mvua kwa kutumia vifaa vya kisasa ambavyo vinawasaidia katika masomo yao, kati kati ni Mkurugenzi wa shule hiyo Sebastian Waryuba.
Na Muhidin Amri,
Songea.

WAHITIMU kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya iliyopo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanatarajia kufanya mitihani yao ya mwisho, Novemba mwaka huu wametakiwa kujiepusha na udanganyifu wa kutafuta majibu ya mitihani hiyo, badala yake watumie muda uliobaki kujisomea ili waweze kufanya vizuri na kufaulu kwa kupata alama za juu.

Aidha wameelezwa kuwa, serikali tayari imejipanga kudhibiti vitendo hivyo ili kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia hiyo na kwamba wameshauriwa kutumia muda huu mfupi uliobakia, kujikumbusha yale waliyosoma na kufundishwa na walimu wao ili siku ya mwisho ya mitihani yao waweze kufuzu vigezo husika.

Ofisa elimu sekondari katika Manispaa hiyo, Leo Mapunda alisema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi, walimu na wazazi katika mahafali ya saba kidato cha nne, shule ya sekondari Beroya yaliyofanyika juzi mjini hapa.


Alisema kuwa, siri ya mwanafunzi kufanya vizuri katika masomo na mitihani yake ni kujiandaa kwa kusoma kwa bidii anapokuwa shuleni na nyumbani, kwa kuzingatia mambo anayofundishwa na walimu wake na sio kukaa na kusubiri kupata majibu kwa njia haramu, jambo ambalo wengi wao linawakwamisha kufikia ndoto yao.

Mapunda alifafanua kwamba, kitendo cha kuzingatia yale yanayofundishwa darasani kunamwezesha mtoto kujiamini katika kujibu mitihani yake ya mwisho kwa ubora wa hali ya juu, na wale ambao wamezoea kutumia njia za mkato hubaki wakihangaika kutafuta majibu ya mitihani, kutoka kwa matapeli ambao huibuka kwa wingi pale mitihani inapowadia kufanyika.

“Leo ninyi vijana wangu mnaomaliza kidato cha nne napenda kuwaeleza kwamba, siri kubwa ya kufanya vizuri katika mitihani ni kusoma kwa juhudi na maarifa ya hali ya juu, ili siku ya mwisho muweze kujibu mitihani yenu vizuri pasipo shaka”, alisema Mapunda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo Sebastian Waryuba alisema kuwa kwa muda wa miaka minne sasa vijana hao wamefundishwa misingi muhimu ambayo kama wataizingatia na kuyafanyia kazi, wataweza kufanya vyema katika mitihani yao na hata katika maisha yao ya kila siku huko waendako.

Waryuba aliwataka pia watoto hao wasibweteke na elimu ya kidato cha nne ambayo wameipata, badala yake iwe mwanzo wa kujiendeleza zaidi jambo ambalo litaweza kukamilisha ndoto ya maisha yao.

Aliwataka kwenda kuwa mfano mzuri katika jamii, ili watu wengine waweze kuiga mambo mazuri kutoka kwao badala ya kushiriki katika matendo maovu ambayo hayaleti picha nzuri, kwao na jamii kwa ujumla.




No comments: