Friday, September 18, 2015

MACHANGUDOA SONGEA WATAFUTIWA DAWA

Mji wa Songea uliopo mkoani Ruvuma.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

OPARESHENI kabambe wakati wowote kuanzia sasa, huenda ikafanyika katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, kwa lengo la kuwasaka na kuwakamata wasichana wanaofanya biashara ya kuuza miili yao, maarufu kwa jina la Machangudoa ambao huzurura nyakati za usiku kwenye mitaa mbalimbali ya mji huo.

Imeelezwa kuwa hatua hiyo itachukuliwa ikiwa ni lengo la kuunga mkono, mkakati wa serikali juu ya kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema kuwa zoezi hilo litafanywa na askari kanzu huku akiyataja maeneo yaliyoathirika zaidi kuwa ni mtaa wa Delux One, Ikweta, Serengeti, Majengo na maeneo ya Mfaranyaki ambako kuna idadi kubwa ya vijana wanaohusika kufanya vitendo hivyo.


“Tumepata taarifa na malalamiko kutoka kwa raia wema kwamba, biashara ya ngono katika mji wetu wa Songea inazidi kuongezeka sasa tumejipanga kufanya msako mkali tuwakamate wale wote wanaoendekeza matendo haya machafu, tumesikia baadhi yao kuna watoto wa watu maarufu hata hivyo tutawakamata wote bila kujali yeye ni nani na ametoka wapi”, alisema Msikhela.

Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona biashara hiyo inazidi kushika kasi mjini hapa, hasa katika nyumba za starehe ambako watu hufanya ngono bila kificho na endapo hali hiyo itaachwa bila kudhibitiwa, ongezeko la maambukizi mapya ya Ukimwi yatazidi kuongezeka na kuhatarisha kupoteza nguvu kazi ya taifa hili.

Msikhela alibainisha kuwa hata watoto wadogo wanaosoma shule za msingi na sekondari, nao wamekuwa wakiacha kuzingatia masomo yao darasani na kwenda kushiriki kufanya biashara hiyo haramu.


Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi hapa mkoani Ruvuma, alifafanua kuwa uchunguzi uliofanywa na Jeshi hilo umebaini pia kuongezeka kwa vitendo hivyo kunatokana na kuwepo kwa vyuo vingi, katika Manispaa ya Songea.

No comments: