Thursday, September 3, 2015

LOWASSA: NITAKAPOINGIA MADARAKANI WALIOHUSIKA KUPANDA KWA DENI LA TAIFA NITAWAFIKISHA MAHAKAMANI

Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

EDWARD Lowassa ambaye ni mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hapa nchini, ambaye pia anawakilisha vyama vyote vya siasa vinavyounda umoja wa katiba wa wananchi (Ukawa) amesema atakapoingia madarakani atahakikisha analifanyia kazi suala la kupanda kwa deni la taifa na endapo atabaini kwamba kuna makosa yalifanyika juu ya kupanda kwa deni hilo, wale wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Nitawafikisha Mahakamani wale wote waliohusika katika jambo hili, ili waweze kulipa fedha walizotumia vibaya kinyume na taratibu za nchi, haiwezekani mzigo huu watishwe watanzania ambao ni maskini na wenye kipato cha chini”, alisema Lowassa.

Mgombea huyo wa Ukawa alisema hayo alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika jana kwenye uwanja wa shule ya msingi Kiwanjani uliopo mjini hapa.

Aidha alisema kuwa endapo ataingia Ikulu ataondoa ushuru wote wa mazao ambao wananchi wamekuwa wakitozwa, kwa kile alichoeleza kuwa nchi ya Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika vizuri hakuna haja ya kuwasumbua wakulima kwa kuwakopa mazao yao na kuwatoza ushuru mdogo mdogo.


Vilevile alieleza kuwa anatambua kwamba, Halmashauri nyingi za wilaya hapa nchini kumekuwa ukifanyika ubadhirifu mkubwa wa fedha za wananchi hivyo atakapoingia madarakani, atawawajibisha kwa namna moja au nyingine wale wote waliohusika katika kufanya hivyo.

“Nimekuja hapa Mbinga ndugu zangu nawaomba kura zenu nyingi za ndiyo ili niweze kuingia madarakani, hawa wezi katika Halmashauri nitakula nao sahani moja, watanitambua na wataona chamtemakuni wengi wenu hapa mnanitambua mimi ni mtu mwenye maamuzi magumu, sitaki serikali nyoro nyoro nataka iwe yenye watu waaminifu na wachapa kazi bora katika kuwatumikia watanzania”, alisema.

Pamoja na mambo mengine aliyekuwa Waziri mstaafu wa mambo ya ndani, Lawrence Masha ambaye naye alikuwa kwenye msafara huo wa kampeni alisema yeye alichukua jukumu la kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda CHADEMA, kutokana na kubaini kuwa ina viongozi ambao wamekigeuza chama hicho kuwa taasisi ya watu binafsi ambayo huwanufaisha matumbo yao na kuacha kuzingatia matakwa ya wananchi, waliowaweka madarakani.

Masha alisema kuwa umefika wakati sasa watanzania wanapaswa kutambua kuwa kilichobaki ni kufanya maamuzi magumu, Oktoba 25 mwaka huu kwa kukichagua CHADEMA ili kiweze kuwaletea maendeleo.

“Lakini nataka niwaambie serikali ya mheshimiwa Lowassa na serikali ya Ukawa, itakuwa inatawala kwa misingi ya haki bila uonevu, hatma ya nchi yenu ndugu zangu watanzania maamuzi yote yapo mikononi mwenu,

“Tumebakiza siku chache kupiga kura, msikubali kutishwa kwa maneno eti kwamba mkiichagua ukawa nchi haitatawalika na misaada ya nje mtaikosa, hao watakaowaambia haya maneno muwapuuze tutahakikisha rasilimali za nchi hii zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi”, alisema Masha.


Hata hivyo baada ya kumaliza mkutano huo wa kampeni hapa wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, mgombea wa Urais Lowassa ambaye anafanya mikutano yake kutoka wilaya moja kwenda nyingine akitumikia Helkopta, alielekea wilaya ya Namtumbo mkoani humo na Sumbawanga mkoa wa Rukwa.

No comments: