Friday, September 11, 2015

CCM TUNDURU YAIRUSHIA KOMBORA VYAMA VYA UPINZANI

Na Muhidin Amri,
Tunduru.

SIKU chache baada ya Chama cha wananchi (CUF) wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kuanza kampeni za wagombea wake wa ubunge katika Jimbo la Tunduru kaskazini na kusini, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na kueleza kuwa wagombea waliosimamishwa na chama hicho cha wananchi hawana uwezo na wasitegemee kupata kura za ushindi, badala yake wagombea wa chama cha mapinduzi ndio watakaoweza kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

CCM imedai kwamba wagombea waliowekwa na chama hicho, Dustan Majolo Tunduru kaskazini na Thabiti Bakiri Jimbo la Kusini ni mteremko kwa chama hicho tawala kuelekea kupata ushindi, ambapo kinawafananisha wagombea hao sawa na kumsukuma mtu mlevi ambaye hana uzito wa kujizuia wakati anaposukumwa, kwa kile walichoeleza kuwa hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana vyama hivyo viliangukia pua.

Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wa wilaya hiyo, Juma Khatibu alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini Tunduru, ambapo alidai kuwa wagombea hao ni dhaifu kisiasa na hawana uwezo wa kukidondosha chama hicho cha mapinduzi.


Alisema kuwa kutokana na wagombea hao kutokomaa vizuri kisiasa, hata hawana mvuto katika jamii ambao ungeweza kuwasaidia kujenga ushawishi wa wananchi wa majimbo hayo, ili wachaguliwe hivyo kufuatia hali hiyo wajiandae kulia tena kama ilivyo kwa uchaguzi mkuu uliopita.

Khatibu alitamba kwamba yeye akiwa kiongozi wa Jumuiya hiyo ya vijana wilayani Tunduru, kwa kushirikiana na vijana wenzake watahakikisha majimbo yote mawili ya uchaguzi wilayani humo, yanarudi mikononi mwa CCM.

Alisema wanaimani kubwa ya kushinda kwa kishindo kutokana na kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana, ambapo kati ya vijiji 153 chama cha mapinduzi kiliibuka mshindi wilayani humo kwa kunyakua viti 115, chama cha wananchi CUF kilipata viti 37 na CHADEMA kiliambulia kiti kimoja.

Kw mujibu wa Khatibu alibainisha kuwa hata katika uchaguzi wa vitongoji, bado CCM iliongoza kwa kufanya vizuri ambapo viti 1006 kati ya 1200 na mafanikio hayo yalitokana na mshikamano uliooneshwa na vijana wa chama hicho tawala, ambao waliweza kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

No comments: