Wednesday, September 23, 2015

MADEREVA WA PIKIPIKI MBINGA WAPEWA SOMO

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa Polisi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Ramia Mganga amewataka madereva wanaoendesha pikipiki wilayani humo, maarufu kwa jina la Yebo yebo kuacha kutumiwa vibaya na wanasiasa, jambo ambalo linahatarisha usalama wao na kusababisha malumbano yasiyokuwa ya lazima.

Aidha alikemea kitendo cha madereva hao baadhi yao kuleta vurugu, kuchoma moto bendera za vyama na kubandua mabango ya wagombea hao katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi, ambayo yamebandikwa katika maeneo mbalimbali jambo ambalo amewasihi kwa kuwaeleza kitendo hicho waachane nacho, kwani husababisha na kuleta mifarakano au mipasuko katika jamii.

Mganga alisema hayo alipokuwa akizungumza na baadhi ya waendesha pikipiki wa wilaya hiyo, katika viwanja vya eneo la stendi kuu ya magari ya abiria mjini hapa.


Kadhalika aliwataka kutii sheria za nchi bila shuruti, ambapo kwa yule atakayeonekana anakiuka atachukuliwa hatua, ili kuweza kudhibiti hali hiyo na kutoweza leta madhara kwa wengine.

“Nawataka tujenge ushirikiano, itikadi zenu za vyama vya siasa isiwe chanzo cha vurugu na kuhatarisha usalama wa wengine tufanye kazi zetu kwa amani, tusikubali kutumiwa na wagombea wa chama fulani ambao wamekuwa wakiwatuma mfanye jambo, kwa maslahi yao na kutaka kuleta machafuko”, alisema Mganga.


Kadhalika kwa upande wao madereva hao wa pikipiki, nao kwa nyakati tofauti walimhakikishia Mkuu huyo wa Polisi wilaya ya Mbinga kwamba wapo tayari kujenga ushirikiano wa pamoja na Jeshi la Polisi wilayani humo, kwa kutoa taarifa pale itakapoonekana kuna tatizo au uhalifu wa aina fulani ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa haraka, kabla ya kutokea madhara.

No comments: